Mchezo wa VPL kati ya mahasimu wa jadi, Yanga na Simba umemalizika kwa timu hizo kumaliza dakika 90 kwa kutoka sare ya bao moja na moja, Yanga ikiwa ya kwanza kupata goli katika dakika ya 26 kupitia kwa Amissi Tambwe na Simba ikisawazisha goli hilo katika dakika ya 87 kupitia kwa Shiza Kichuya.
Aidha mchezo huo umeshuhudiwa mashabiki wa Simba wakivunja viti vya Uwanja wa Taifa kwa kumlaumu mwamuzi Juma Mgunda kuwa goli lililofungwa na Tambwe halikuwa sahihi kwani Tambwe alishika mpira kwa mkono kabla ya kufunga na pia tukio hilo lilipelekea nahodha wa Simba, Jonas Mkude kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumpiga ngumi mwamuzi.
Pia Simba imeendeleza rekodi ya msimu wa 2016/2017 kwa kutokufungwa mchezo hata mmoja kati ya michezo saba iliyocheza mpaka sasa, ikishinda mitano na kutoa sare mwili, kama utakuwa na kumbukumbu nzuri, msimu ulipita Simba ilipoteza mchezo wa saba ilipokutana na Yanga na kufungwa goli 2-0.
Kwa matokeo ya mchezo wa Yanga na Simba, Simba sasa imefikisha alama 17 ikiwa kileleni kwa msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Yanga ikifikisha alama 11 ikiwa katika nafasi ya tatu ya msimamo wa VPL.
Dondoo muhimu
- Mkude ni mchezaji wa pili wa Simba kuoneshwa kadi nyekundu katika mechi mbili za mwisho za Simba vs Yanga, Mechi ya iliyopita ya Simba vs Yanga Abdi Banda alioneshwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza katika mchezo ambao Yanga walishinda 2-0.
- Amis Tambwe amefunga magoli matatu katika mechi tatu mfululizo za mwisho za Simba vs Yanga. Alifunga goli moja katika kila mechi za msimu uliopita kabla ya kufunga kwenye mchezo wa leo.
- Simba na Yanga zilikuwa zinakutana kwa mara ya 93 katika historia ya ligi kuu Tanzania bara, sare ya mchezo huo inafanya timu kutoka sare katika jumla ya mechi 33. Yanga inaongoza kwa kushinda mechi 35 ikiwa imefunga magoli 102 wakati Simba imepata ushindi katika mechi 25 na kufunga magoli 89.
- Simba imeendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo msimu huu, imecheza mechi saba na kufanikiwa kushinda mechi tano na kutoka sare mara mbili. Yanga imecheza mechi sita, imeshinda mechi tatu, imetoka sare mara mbili na kupoteza mchezo mmoja.
- Simba bado inaongoza ligi ikiwa na pointi 17 ikifuatiwa na Stand United ambayo inapointi 12 huku Yanga wakishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 11.
- Juma Mahadhi, Vicent Andrew ‘Dante’ ni wachezaji wa Yanga ambao wamecheza kwa mara ya kwanza Kariakoo derby wakati kwa upande wa Simba walikuwa ni Janvier Bokungu, Method Mwanjale, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon na Mohamed Ibrahim.
- Kichuya amefunga magoli matano kati ya 13 ambayo tayari Simba imefunga hadi sasa huku Amis Tambwe akiwa ndio mfungaji mwenye magoli mengi hadi sasa, amefunga magoli manne kwenye mechi sita alizoichezea Yanga.
- Simba ndiyo inaongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye ligi hadi sasa ikiwa imeshazamisha kambani jumla ya magoli 13 wakati Yanga wao wamefunga magoli 9 huku wakiruhusu kufungwa magoli mawili.
0 comments:
Post a Comment