Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema timu aliyoiunda ichunguze tuhuma za ubadhirifu kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) imekamilisha kazi yake na imebaini madudu mengi zaidi.
source:http:hivisasa.co.tz
Majaliwa ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Aprili 15, 2017) wakati akizungumza na wajumbe zaidi ya 300 wa mkutano wa wadau wa zao la tumbaku katika ukumbi wa Kiyungi mwana Isike, Mjini Tabora.
“Nilikuja Tabora mara ya kwanza ili kuchukua hatua za dharura na leo nimekuja kuendelea na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwezesha kilimo cha tumbaku kiwe na tija kwa wakulima na ndiyo maana niliomba wakulima, wanunuzi wa tumbaku, vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) na viongozi wa Serikali wawepo kwenye mkutano huu,” amesema.
Akitoa mrejesho juu ya uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda, Waziri Mkuu amesema WETCU haikuwa na kitengo cha ununuzi kwa zabuni.
“Waliunda kampuni inayoitwa FDTU (Flu and Dark Tobacco Union) ambayo ni Umoja wa Wenyeviti wa Union zote za Tumbaku nchini ambayo ilipewa kazi zote za ununuzi wa pembejeo na hela walikuwa wanagawana,”amesema.
“Tumefanya ufuatiliaji hadi katika benki lakini kwenye akaunti hakuna hela mpaka sasa. Tumeangalia chanzo cha fedha za union zenu na kubaini hakuna fedha zinazotoka FDTU kwenda WETCU,” ameongeza.
Akifafanua kuhusu kashfa ya ununuzi wa gari aina ya shangingi lenye namba za usajili T181 DEN ambao ulifanywa kinyume na maazimio ya mkutano mkuu, amesema viongozi wa WETCU walitumia zaidi ya Shilingi milioni 220 kuzidi kiwango kilichoidhinishwa na Mkutano Mkuu cha kununua gari lenye thamani ya Shilingi milioni 40.
“Gari walilolinunua ni la mwaka 2008 na siyo la mwaka 2015 kama taarifa zinavyoonesha. Lilikwishatumika kwa kilometa zaidi ya 95,000 lakini likarekebishwa hadi kubakiza kilometa 16,000 ili lionekane ni jipya,… maana yake wamekula fedha nyingi sana na ni lazima tuwachukulie hatua za kisheria kwa sababu wamekula fedha, wamenunua gari lililotumika na siyo maamuzi ya mkutano mkuu,” amesema.
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment