Sunday, April 16, 2017

MAELFU YA WANANCHI KIGOMA KUTIBIWA MACHO BILA MALIPO

Mamia ya wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya mkoa wa Kigoma, wamejitokeza na wengine wakiendelea kuwasili katika kijiji cha Ilagala wilayani Uvinza kwa ajili ya kupata huduma ya vipimo na matibabu ya macho inayotolewa bila malipo na taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania.


Kwa muda wa siku nne taasisi ya Bilal Muslim, itatoa huduma ya upasuaji wa macho, kutoa miwani ya macho bure ili kuwasaidia watu wenye uoni hafifu kuona vizuri na kutibu tatizo la mtoto wa jicho, ambapo katika siku ya kwanza tu zaidi ya watu hamsini wakiwemo watoto wametibiwa tatizo la mtoto wa jicho.
Martibu wa Kambi za Macho kutoka Bilal Muslim Mission of Tanzania, Ain Sharriff, amesema katika kipindi cha siku nne wanatarajiwa kuhudumia watu 5000 na kufanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu 200.
Wachache miongoni mwa waliopata hudumu na kupata ufumbuzi wa matatizo yao ya macho wameishukuru taasisi ya Bilal Muslim Mission kwa kutoa matibabu bure huku Diwani wa Kata ya Ilagala, Kafunya Kassim akieleza kuwa Bilal Muslim Mission wamefanya jambo jema kupeleka huduma hiyo kwa wananchi walioko vijijini ambao kwa kawaida sio rahisi kuipata.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Bilal Muslim Mission barani Afrika, Mokhsin Mohamed Abdallah,ameeleza madhumuni ya kuweka kambi ya macho kuwa ni kusaidia serikali pale inapoishia katika kufikisha huduma za kiafya kwa wananchi wengi wa vijijini walio mbali na wasioweza kumudu gharama za matibabu.
“Serikali imejitahidi, imeweka vituo vya afya, imeweka zahanati lakini hizo zina daraja zake ambazo hazijafikia uwezo wa kufanya tiba zingine kubwa kubwa ambazo tunaweza sisi wengine kusaidia taasisi tofauti tofauti kuweza kuleta mafanikio kwa wananchi ili watibiwe,”alisema Mokhsin Mohamed abdallah.
Katika hatua nyingine amekosoa viongozi wa mkoa wa Kigoma kwa kuwa wachoyo wa fadhila na kutotambua mchango wa wadau wa maendeleo ya kijamii walau hata kutoa shukrani kwa kwa juhudi zinazofanywa na wadau husika ikilinganishwa na mikoa mingine.
Akiongea katika uzinduzi wa kambi ya macho katika kijiji cha Ilagala, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Alhaji Sheikh Hassan Kiburwa, ameishukuru taasisi ya Bilal Muslim, kwa kusaidia watu wenye matatizo huku akitoa wito kwa wananchi wengi zaidi kujitokeza.
Mbali na kutoa matibabu Taasisi ya Bilal Muslim Mission, inachukua takwimu na kuzituma wizara ya afya ili serikali iweze kuona ukubwa wa tatizo na kuweka mipango ya kusaidia wananchi.

source:dewjiblog
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment