WALIMU 8,955 wamepewa mafunzo na mbinu za kuchambua mtaala mpya ulioboreshwa na uimarishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la tatu na la nne nchini.
Naibu Waziri Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya, alitoa takwimu hizo mjini hapa juzi wakati akiahirisha mafunzo ya mtaala ulioboreshwa na kuimarisha Stadi za KKK kwa walimu wa darasa la tatu na la nne wanaofundisha hisabati, Kiswahili na Kiingereza mkoani Dodoma.
Akiahirisha mafunzo hayo wilayani Kondoa, Manyanya alitaja mikoa yote inayoyatoa kuwa ni Dodoma kwa walimu 1,456, Kigoma (1,270), Lindi (994), Mara (1,545), Shinyanga (1,128), Tabora (1,530) na Simiyu (1,032).
Alisema katika kipindi cha mwaka jana mafunzo hayo pia yalitolewa kwa walimu 22,993 kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Geita, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya na Morogoro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Singida, Songwe na Tanga.
Manyanya alipongeza Wakala wa Usimamizi wa Maendeleo ya Elimu Nchini (ADEM), ambaye ndiye mfadhili wa mafunzo hayo, kutokana na kazi nzuri anayofanya ya kuimarisha usimamizi na uthibiti wa ubora wa elimu nchini.
Kwa mujibu wa Manyanya, pamoja na ADEM kufadhili mafunzo hayo, wizara kupitia wakala huo imetoa mafunzo yanayohusu mtaala ulioboreshwa na stadi za KKK kwa wathibiti wa ubora wa shule.
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment