SERIKALI ya Mkoa wa Dar es Salaam inakusudia kuzivunja nyumba zote zilizopo katika eneo la Manzese, eneo maarufu kama Uwanja wa Fisi, kata ya Tandale, Manispaa ya Kinondoni kutokana na kukithiri kwa biashara haramu katika eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, ameyasema hayo wakati alipotembelea eneo hilo maarufu kwa madanguro na kujionea hali halisi ya eneo hilo.
Makonda alisema eneo hilo limekuwa maarufu kwa biashara haramu hivyo serikali imedhamiria kubadilisha eneo hilo ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vidogo vidogo.
"Kuanzia sasa sitaki kuona biashara hizo mbovu zikiendelea pabomolewe sababu nimepata taarifa Mkuu wa Wilaya una mpango wa kununua na kupaendeleza sasa nataka pabadilike, "amesema Makonda.
Akiwa katika eneo hilo Makonda alijaribu kugonga milango ya vyumba ambavyo inahisiwa kuna wasichana wanaojiuza lakini haikufunguliwa.
Baadhi ya watu waliokuwa nje ya vyumba hivyo, wakinywa pombe za kienyeji walidai kuwa katika vyumba hivyo kulikuwa na watu na kwamba huduma zilikuwa zikitolewa.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amemwambia Makonda kwamba eneo hilo ni maarufu kwa wasichana kujiuza na baadhi ya wazazi wamewaruhusu mabinti zao kufanya biashara hiyo haramu na tayari wameshapiga marufuku kuendelea kwa biashara hizo.
“Hapa watu wanakunywa pombe muda wote. Iwe asubuhi, mchana hadi usiku tayari tuna mpango wa kupaendeleza,” amesema Hapi.
Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
0 comments:
Post a Comment