Thursday, October 6, 2016

Tanzania kupata ruzuku na mkopo wa Dola Bilioni 1.6 kutoka Benki ya Dunia


Benki ya Dunia inakusudia kuipatia Tanzania ruzuku na mkopo wenye masharti nafuu wa dola Bilioni 1 nukta 6 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 3 nukta 5 kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo nishati ya umeme, kilimo biashara na ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu amesema Jijini Washington DC, Marekani ambako Ujumbe wa wataalamu wa masuala ya uchumi na Fedha kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kwamba mazungumzo kuhusu mkopo huo yako katika hatua za mwisho.
Prof. Ndulu amesema kuwa upatikanaji wa mkopo huo utaisaidia serikali kuboresha miundombinu yake mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya sekta ya viwanda kwa kuimarisha pia mazingira ya sekta binafsi kufanyabiashara na kuwekeza mitaji na teknolojia.
“Mbali na mkopo huo ambao ni muhimu kwa taifa, tunajadili pia namna ukuaji wa uchumi unavyotakiwa kuakisi maisha ya kawaida ya wananchi wetu kwa kupiga hatua kimaisha na kuondokana na umasikini,” alisema Gavana Prof. Ndulu.
Aidha, amesema kuwa Benki ya Dunia imesifu hatua zilizofikiwa na serikali ya Tanzania katika kukuza na kusimamia uchumi wake ambao licha ya uchumi wa dunia kushuka viwango vyake vya ukuaji uliotarajiwa wa asilimia 3.3 na kukua kwa asilimia 1.5 tu, Uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia 7.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zinazoendelea ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na unatarajia kukua zaidi kutokana na kuvumbuliwa kwa gesi na kushuka kwa mfumuko wa bei” Alisisitiza Prof Ndulu
Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa mkopo utakao tolewa ni pamoja na dola milioni mia 2 kwaajili ya kulijengea uwezo shirika la ugavi wa umeme nchini Tanzania-Tanesco ili liondokane na nakisi inayosababishwa na madeni makubwa yanayolikabili shirika hilo
Dkt. Mpango Amefafanua kuwa mkopo huo pia utaiwezesha serikali kulipa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kufanyika kwa uhakiki wa kina wa madeni hayo ili kuiwezesha mifuko hiyo itoe huduma inayostahili kwa wananchama wake.
Amesema kuwa kiasi kingine cha fedha hizo kitatumika kuijengea uwezo sekta binafsi iweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Taifa pamoja na kuimarisha kilimo kwa kuwawezesha wakulima kulima kilimo cha kibiashara na kuondoa kodi zenye kuleta kero katika sekta ya kilimo.
“Wakati tunatekeleza mpango huo tutaangalia pia namna ya kupitia upya kodi zinazolalamikiwa katika sekta ya utalii” amefafanua Dkt. Mpango
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Mohamed, ameishukuru Benki ya dunia kwa kuisaidia nchi hiyo kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa visiwani humo ikiwemo uboreshaji wa rasilimali watu, miundombinu ya barabara, kiwanja cha ndege na kuboresha mazingira yatakayochangia kukua kwa sekta ya utalii visiwani humo.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Makhtar Diop, amesema kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania ili iweze kufanikiwa kiuchumi na kijamii.
Amesifu juhudi na hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha nidhamu ya kazi na kupambana na vitendo vya ufisadi hatua ambayo inaungwa mkono na benki yake ili kuharakisha maendeleo ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.
Diop amebainisha kuwa Benki yake inataka kuona Shirika la Umeme Tanzania Tanesco linaboreshwa na kuwa la kisasa kwakuwa nishati ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa viwanda na kwamba wangependa kusaidia eneo hilo namengine ya kuboresha rasilimali watu kwa kuwekeza kwenye elimu na kuwainua wananchi kimapato kupitia mradi wa TASAF na mingine itakayoanzishwa.

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video 

0 comments:

Post a Comment