Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila Kabange leo tarehe 04 Oktoba, 2016 wamefanya mazungumzo rasmi Ikulu Jijini Dar es Salaam na kisha kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo viongozi hao wawili wamekubaliana kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria katika nchi hizi mbili marafiki na majirani.
Akizungumza Rais Kabila amesema Kongo inatambua umuhimu wa kushirikiana na Tanzania katika biashara na uwekezaji na kwamba amefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Tanzania imezichukua kuboresha huduma katika bandari ya Dar es Salaam ambayo ni tegemeo kwa usafirishaji wa mizigo ya Kongo Mashariki na sehemu nyingine za nchi hiyo.
Ameahidi kuwa pamoja na kuwahasisha wafanyabishara wa Kongo kuitumia bandari ya Dar es Salaam, Serikali yake itachukua hatua za kurekebisha kasoro zinazolalamikiwa na wafanyabiashara dhidi ya maafisa wa forodha wa Kongo waliopo hapa nchini.
Rais Kabila amezungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania akisema nchi yake pia imeamua kutumia bomba hilo kusafirisha mafuta yake iliyoyagundua katika ziwa Albert upande wa Kongo na pia juhudi zinazoendelea kupata mafuta katika ziwa Tanganyika na amesisitiza kuwa ili kufanikisha hilo ushirikiano ni muhimu.
Kuhusu hali ya usalama nchini Kongo, Rais Kabila amesema kwa asilimia 97 nchi hiyo ina usalama na kwamba ni maeneo machache tu ya mashariki mwa Kongo ndiko kuna vikundi vinavyoendesha vurugu.
‘Mhe. Rais Magufuli hivi karibuni tutaanza mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu nchini Kongo, na lengo letu ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Desemba ama baada ya mwezi Desemba” amesema Rais Kabila’
0 comments:
Post a Comment