Wednesday, April 5, 2017

Watumiaji petroli kupumua

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kuwa bei ya mafuta ya dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo imepanda huku bei ya petroli ikipungua kwa Sh tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlagosi, Meneja Mawasiliano na Uhusiano, Titus Kaguo alisema bei ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh saba sawa na asilimia 0.36 wakati bei ya dizeli imepanda kwa Sh 12 kwa lita sawa na asilimia 0.63.
Kaguo alisema kutokana na kupanda huko kwa bei hizo, mafuta ya taa sasa yatauzwa Sh 1,858 kutoka Sh Sh 1,852 huku dizeli ikuzwa Sh 1,925 kutoka Sh 1,913 kwa lita.
Alifafanua kuwa mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yametokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, mfumuko wa bei na gharama za usafirishaji ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa mafuta yanayoshushiwa mkoani Tanga pamoja na kwamba hakuna meli iliyoshusha mzigo wa mafuta katika bandari hiyo, nako bei ya mafuta kuanzia leo itapanda kwa aina zote tatu za mafuta kwa Sh saba.
Alisema hali hiyo imetokana na hatua iliyochukuliwa na Ewura katika kuwasaidia wafanyabiashara wa mafuta kupambana na tatizo la mfumuko wa bei kwa kuwaongezea Sh tatu katika faida wanazopata.
Alisema Watanzania wanaweza kufuatilia bei za mafuta kulingana na eneo au mkoa wanaotoka ama kwenda kupitia namba *150*#.
Alisisitiza kuwa kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi tu bei hizo ziwe chini ya bei kikomo zilizotolewa na mamlaka hiyo baada ya kuzikokotoa kwa mujibu wa kanuni ya kukokotoa bei za mafuta.
Aliwakumbusha wamiliki wa vituo vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei hizo za mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment