Wednesday, April 5, 2017

TRA YAKUSANYA TRILIONI 10.87

Ukusanyaji mapato katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Juni 2016 hadi Machi 2017 umeongezeka kwa asilimia 9.99 kutoka trilioni 9.88 kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha wa 2015/16 hadi trilioni 10.87 kwa mwaka huu wa fedha.

Wakati akitoa taarifa za makusanyo ya kodi kwa waandishi wa habari Aprili 4,2017, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo amesema mamlaka hiyo itaelekeza juhudi zake katika kukusanya kodi mbalimbali ili kuhakikisha lengo la mwaka la kukusanya trilioni 15.1 linafikiwa.
“Katika mwezi wa Machi 2017 TRA imekusanya jumla ya shilingi trilioni 1.34 ukilinganisha trilioni 1.31 ya mwezi machi 2016 ambayo ni sawa na aslimia 2.23. Pamoja na mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, katika kipindi cha miezi mitatu kilichobaki TRA itahakikisha inakusanya kodi mbalimbali ili kufikia lengo la kukusanya trilioni 15.1 kwa mwaka,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kayombo amesema TRA inaendelea na mpango wake wa kukusanya kodi za majengo kwa kutoa viwango maalumu vya kodi kwa majengo ambayo bado hayajafanyiwa tathimini.
“Wamiliki wa majengo ambayo bado hayajafanyiwa tathimini wanajulishwa kufika katika ofisi zetu za mikoa au kutembelea tovuti ya TRA kuangalia viwango hivyo,” amesema na kuongeza.
“Vile vile tunasisitiza kuwa matumizi ya EFD pamoja na zoezi la uhakiki wa TIN katika baadhi ya mikoa linaendelea hivyo wananchi wanaombwa kuhakikisha wanatumia mashine hizo na wale wa mikoani wanahakiki TIN namba zao.”


Source:dewjiblog
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment