Wednesday, April 12, 2017

Nukuu 20 za Rais Magufuli wakati akizindua ujenzi wa reli ya kisasa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli Jumatano hii, amefanya uzinduzi wa reli ya kisasa, Standard Gauge Railway(SGR LINE). Wakati wa uzinduzi huo Rais Magufuli amesema ujenzi huo utakuza sekta zingine nchini huku hadi kukamilika kwake ikitarajiwa kutoa ajira takribani milioni 1.
Uzinduzi huo wa reli ya umeme, umehudhuriwa pia na mawaziri na baadhi ya mashirika yaliyosaidia ujenzi huo pamoja na wananchi.
“Ujenzi wa reli huwa ni gharama kubwa, reli hii itakuwa inabeba uzito mkubwa na spidi kubwa, watu watalala Moro na watafanya kazi Dar es Salaam na ujenzi huu wa reli ya kisasa utakuza sekta zingine nchini, itawezesha malighafi mbalimbali kusafirishwa kwenda kwenye maeneo ya viwanda,” alisema Rais Magufuli.
Hizi nukuu 20 za Rais Magufuli katika hotuba yake kwenye uzinduzi huo:
1.Niwaombe tuangalie Tanzania kwanza siasa baadaye, muiache serikali ya CCM iliyoaminiwa na Watanzania itekeleze wajibu wake tutakutana 2020
2.Watanzania wanataka maendeleo, hakuna anayekula siasa kwa hiyo Tanzania kwanza siasa baadae
3.Tanzania tunaweza kwa hiyo tunapoyafanya haya tunafanya kwa sababu tuna wajibu wa kufanya, na haya ni malipo yangu kwenu
4.Niko kwa niaba yenu, tumeonewa sana, Tanzania ni tajiri hatutakiwi kuwa ombaomba
5.Mlinituma nifanye haya, au niwaulize ndugu zangu haya yote ninayoyafanya kweli ni mabaya?
6.Nazuia hata michanga ya madini, ninafanya kazi hii kwa niaba yenu, kwani nashindwa kusema nipelekee hiyo michanga nitaikuta Ulaya?
7.Wanasema samaki mkunje akiwa mbichi, fisadi mkunje akiwa mbichi akishakomaa mvunje, nafuu walalamike wachache, Watanzania wafurahi
8.Vita ya kupambana na ufisadi ni ngumu na hasa unapowabadilisha watu wachache waliozoea maisha fulani kwa miaka 50
9.Nataka mhandisi amalize mradi wa reli ya kisasa kabla ya miezi 30, na ikiwezekana siku ya kufungua twende bure mpaka Dodoma
10.Tunajua tunapoenda pasitokee mtu wa kubadilisha ajenda tuanze kuzungumzia ajenda ambazo hazipo kwenye ilani ya uchaguzi
11.Hivi karibuni tumepata mkopo wa kuanza kujenga barabara za mwendokasi katika awamu ya tatu na ya nne
12.Tanzania imekuwa kwa uchumi 7%, ushahidi wa kukua kwa uchumi ndio hii miundombinu tunayoijenga
13.Kazi tunazozifanya mara nyingi utakaowaona wanapiga kelele ni wale ambao walizoea kupiga dili, na mimi nataka waendelee kupiga kelele
14.Nawahakikishia Watanzania mimi ni dereva mzuri nawahakikishia lori litafika kule tunakokwenda na hili ni lori la maendeleo
15.Wale wataalamu wa kusoma kwenye mitandao wakaangalie ni nchi gani imejenga reli ya namna hii kwa pesa zake watakuta ni Tanzania
16.Mradi huu wa ujenzi wa reli ya kisasa unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 30
17.Mradi huu wa ujenzi wa reli ya kisasa unatarajiwa kutoa ajira kwa watu takribani milioni 1
18.Ujenzi wa reli hii ya kisasa utasaidia kutunza barabara zetu, barabara zetu zinaharibika kwa sababu zinasafirisha mizigo mikubwa
19.Ujenzi wa reli ya kisasa utakuza sekta zingine nchini, itawezesha malighafi mbalimbali kusafirishwa kwenda kwenye maeneo ya viwanda
20.Ujenzi wa reli huwa ni gharama kubwa, reli hii itakuwa inabeba uzito mkubwa na spidi kubwa, watu watalala Moro na watafanya kazi Dar es salaam
Na Emmy Mwaipopo


Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment