RAIS John Magufuli amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird na wamezungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania, yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.6, zikiwa ni mkopo kutoka benki hiyo.
Akizungumza baada ya kumaliza mazungumzo yake jana na Rais Magufuli, Bird alisema mikopo hiyo, inalenga kusaidia juhudi za maendeleo nchini Tanzania, na itatolewa katika sekta mbalimbali, zikiwemo nishati, usafirishaji, elimu na maji.
“Miradi hii yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika maisha ya Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na msukumo mzuri kutoka serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia maendeleo,” alisema Bird.
Kwa upande wake, Rais Magufuli aliishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo.
Alitoa wito kwa benki hiyo, kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi. “Tunataka kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi hii ina manufaa makubwa kwa Watanzania na tungependa utekelezaji wake ufanyike haraka, na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa,” alisisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alimhakikishia Bird kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano, imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa sasa na itakayoanza kutekelezwa katika siku zijazo kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia. Kwa hivi sasa, miradi 26 yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 4.5, inatekelezwa hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Source: mtembezi.
0 comments:
Post a Comment