Saturday, November 12, 2016

DK SHEIN – SMZ ITASIMAMIA AFYA TA KINAMAMA NA WATOTO

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha afya za akinamama na watoto zinaimarishwa, ikiwamo kupunguza vifo kwa kuwepo huduma bora na nzuri.

Dk Shein alisema hayo wakati akifungua wodi ya kisasa ya watoto na wajawazito ambazo ujenzi wake umegharamiwa na serikali ya Norway na Uholanzi katika katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini hapa.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo unadhihirisha kwamba sasa nia na malengo ya kupunguza vifo kwa akinamama na watoto vinavyotokana na uzazi yatafikiwa.

Aidha alisema kukamilika kwa majengo hayo kunatoa nafasi kubwa kwa akinamama kujifungua katika hospitali za Serikali na kupata huduma chini ya madaktari bingwa.

Dk Shein alisema katika kipindi cha miaka mitano sasa, huduma za afya katika hospitali ya Mnazi Mmoja zimeimarika kwa kiwango kikubwa ikiwamo kupatikana kwa huduma za upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo ambao umepata ufadhili mkubwa wa Serikali ya Hispania.

Aidha, alisema maabara ya hospitali hiyo inafanya kazi ya utafiti na uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na vipimo vyake, vinatambuliwa kikanda katika nchi za Afrika ya Mashariki.

Alisema huduma za matibabu ya figo na usafishaji wa damu zinatarajiwa kutolewa katika hospitali hiyo hivi karibuni hatua ambayo inakwenda sambamba na kuifanya hospitali hiyo kuwa na hadhi ya rufaa.

Mapema, Dk Shein alisema tumaini lake ni kuwapo kwa huduma za kisasa za wajawazito kwa kiasi kikubwa kutawafanya kujifungua katika kituo hicho chini ya uangalizi wa madaktari bingwa. Alisema takwimu zinaonesha kwamba, mwaka 2010 asilimia 42 ya akinamama walikuwa wakijifungua katika hospitali hiyo na wamefikia asilimia 52 mwaka 2015.



Source:mtembezi

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video



0 comments:

Post a Comment