Friday, October 14, 2016

MAFANIKIO MICHEZONI CHINI YA MWALIMU NYERERE


Kisiasa mabadiliko ya uongozi hufahamika kama “Awamu” ila michezoni mabadiliko ya mashindano hufahamika kama “Msimu”. Katika siku muhimu kama ya leo tunapokumbuka kifo cha Rais wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni wazi hatuwezi kusahau mafanikio ya tasnia ya michezo kwa kipindi hicho.

Katika kudumisha Amani na Mshikamano miongoni mwa jamii, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitumia michezo zaidi katika kuunganisha wananchi huku yeye akipendelea zaidi mchezo wa Bao japokuwa hakukaa mbali na soka pamoja na michezo mingine kama riadha.

Moja ya mafanikio makubwa ya mchezo wa riadha katika utawala wa Nyerere ni pale Mwanariadha Filbert Bayi alipoibuka kinara kwenye michezo ya Commonwealth mwaka 1974 akishinda mbio za mita 1500 nchini New Zealand. Majina kama Suleiman Nyambui hayawezi kusaulika baada ya kutwaa medali ya fedha  mwaka 1980 katika michuano ya Olympic iliyofanyika Moscow katika mbio za mita 5000.


Serikali Awamu ya Nne na Tano zimejitahidi kuboresha miundombinu lakini moja ya changamoto kubwa imekuwa ni kutoimarisha michezo shuleni ambapo Mwalimu alijitahidi kutumia UMISSETA kama njia ya kuibua vipaji shule za sekondari huku UMITASHUMTA ikitumika shule za msingi.

Katika soka hakika ni ngumu kusahau Awamu hiyo ya Kwanza ya kutokana na historia iliyowekwa na timu ya taifa ya soka mwaka 1980 iliposhiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika AFCON nchini Nigeria 1980. Tanzania ilijumuika na timu za Misri, Ivory Coast na wenyeji Nigeria katika kundi A.

Ama hakika Awamu ya Kwanza ya uongozi ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inahesabika kuwa ndio awamu ambayo tasnia ya michezo ilipata mafanikio kuliko awamu yoyote. Hadi sasa hakuna rekodi iliyovunjwa kati ya hizo. Je ni wakati sasa wa kurudi nyuma na kutumia mbinu za Mwalimu katika kuendeleza michezo?



Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video 







0 comments:

Post a Comment