Saturday, October 15, 2016

TCRA YAZUIA SAMSUNG GALAXY NOTE 7 KUUZWA NCHINI

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wafanyabiashara wenye leseni za kuingiza simu nchini, zinazotolewa na mamlaka hiyo, kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Kampuni ya Samsung ya kurejesha simu za kisasa za Samsung Galaxy Note 7 baada ya kubainika zina matatizo ya betri.

Akizungumza Dar es Salaam , Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema ni vyema mawakala hao wakatekeleza maagizo hayo, kwani simu hizo ni hatari kuendelea kutumika.

Aidha Mungy aliwataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua ili kuepusha hatari ambayo tayari Sumsung wameshaitoa.


“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri na mara mbili sasa imelipuka, hakuna faida ya mtu kuendelea kuitumia unaweza ukasababisha hatari kubwa, inapolipuka inaweza kukuondoa mikono, inaweza kulipua nyumba na matatizo mengine tunawataka wenye simu hizo kuziridisha haraka,” alisema Mungy.

Pia alisema simu hiyo haijasambaa hapa nchini, lakini kuna watu wanaweza kuwa wameletewa zawadi au mtu alisafiri na kuamua kuinunua.

“Taarifa tulizonazo haijaingia sana hapa nchini lakini wapo walioletewa kama zawadi kutoka nje ya nchi nawaomba warudishe huko kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” aliongeza Mungy.

Hivi karibuni Samsung ilitangaza kwamba haitaunda tena simu aina ya Galaxy Note 7 baada ya kutokea kwa ripoti kwamba simu ambazo kampuni hiyo iliamini ziko salama, zinawaka moto.

Kampuni hiyo ilikuwa tayari imepunguza uundaji wa simu hizo na iliwataka waliokuwa na simu hizo, kuzizima na kuacha kuzitumia huku uchunguzi ukiendelea.

Samsung iliwataka watu waliokuwa wamenunua jumla ya simu milioni 2.5 mwezi Septemba mwaka huu, kuzirejesha madukani baada ya wateja wengi kulalamika kwamba betri za simu hizo zilikuwa zinalipuka. Katika hatua nyingine, wiki iliyopita, Kampuni hiyo ya Samsung ya Korea Kusini ilitangaza kuwa imesitisha utengenezaji wa simu aina ya Galaxy Note 7.



0 comments:

Post a Comment