Thursday, October 6, 2016

DPP na DCI wakabidhiwa jukumu la kufanya upepelezi wa mauaji ya watafiti, Dodoma


Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kujihusisha kikamilifu na upelelezi wa kesi ya mauaji ya wataalamu wawili wa utafiti wa udongo na dereva mmoja, yaliyotokea hivi karibuni katika kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amesema wizara yake itahakikisha kuwa wote waliohusika kufanya tukio hilo la mauaji wanafikishwa mahakamani.
Na kwamba, Jamhuri itahakikisha inadai adhabu kali kwa kila mtuhumiwa ili kutoa fundisho kwa wananchi wote kwamba tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kigezo cha hasira kali hakifai.
“Ili kukomesha kabisa wimbi hili la wananchi kujichukulia sheria mkononi , wizara itachukua kila hatua inayowezekana kuhakikisa kuwa wote waliohusika kushawishi, kuhamasisha, au kuchochea ,kupanga, kushambulia kwa mapanga na kushiriki kuchoma moto katika tukio hilo wanafikishwa mahakamani kuvuna walichopanda,” amesema.
Dk. Mwakyembe amesema wizara inashtushwa na ongezeko la matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa visingizio mbalimbali.
“Wengi wanafanya matukio hayo kwa visingizio mbalimbali kama kukasirishwa na baadhi ya matukio wanayoyaona mabaya, kuhisi kuonewa, kuchoshwa na michakato halali ya kisheria ya upelelezi, uendeshaji kesi na utoaji hukumu,” amesema.
Amevitaka vyombo vya habari kuisaidia serikali katika kampeni ya kutokomeza vitendo vya wanachi kujichukulia sheria mkononi.
“Wizara inavitaka vyombo vya habari kubadilisha mfumo wa kuripoti matukio kama hayo kwa kuachana na maneno kama wananchi wenye hasira kali ambayo ni kisingizio kinachowafanya baadhi ya watu kufanys matukio hayo,” amesema.

0 comments:

Post a Comment