Monday, May 8, 2017

SAMIA AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MIILI YA WANAFUNZI ARUSHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan leo tarehe 8-May-2017 ameongoza mamia ya wananchi wa mkoa wa Arusha na Mikoa ya Jirani katika kuaga miili ya wanafunzi 32,walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Visent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha waliopata ajali katika eneo la Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha.
Katika hotuba yake kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi katika tukio la kuaga miili hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahakikishia waombolezaji kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na chenye majonzi mazito kwa kuondokewa na wapendwa wao.
Amehimiza wananchi kote nchini kuungana katika msiba uliotokea kwa kuwafiriji wafiwa katika kipindi hiki kigumu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali peponi.
Makamu wa Rais pia ameiagiza Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Jeshi la Polisi nchini,walimu, wazazi na walezi wawe makini katika kuhakikisha kuwa sheria za usalama barabarani zinazingatiwa kwa kuchukua hatua stahiki za kulinda watoto hasa wanapotumia vyombo vya moto kwenye shughuli zao za kimasomo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuepusha matukio ya ajali ambayo yanaweza kuzuilika kote nchini.
Makamu wa Rais amewataka madereva nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani na waache kutumia pombe na dawa za kulevya ili kuepukana na ajali ambazo zinagharimu maisha ya wananchi.
Makamu wa Rais pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta na Wakenya kwa ujumla kwa kuungana na Wananchi wa Tanzania katika msiba uliotokea.
Katika kuaga miili ya wanafunzi, walimu na dereva katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha, Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta amewakilishwa na Waziri wa Elimu wa nchi hiyo Fred Matiang’i.
Ibada na Dua ya kuaga miili hiyo, imehudhuriwa na Mawaziri mbalimbali ikiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mohammed Aboud,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene, Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Viongozi wa vyama vya siasa na Viongozi wa Dini.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais, Arusha


source:dewjiblog
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment