RAIS John Magufuli leo anapokea ripoti ya kamati maalumu aliyoiunda kuchunguza biashara ya usafirishaji makinikia ya shaba maarufu kama ‘mchanga wa dhahabu’ nje ya nchi.
Kamati hiyo iliyo chini ya uenyekiti wa Profesa Abdulkadir Mruma itakabidhi ripoti hiyo baada ya kukamilisha kazi waliyokuwa wamepewa na Rais Magufuli. Ripoti hiyo ndio itatoa majibu ya sintofahamu iliyodumu kwa miaka 19.
Kwa mujibu wa takwimu za TMAA, kila mwaka kontena zaidi ya 50,000 za makinikia zinasafirishwa nje ya nchi, jambo ambalo linafanya tangu mwaka 1998 makontena zaidi ya milioni moja kuwa yameshasafirishwa nje ya nchi.
Rais Magufuli aliunda kamati hiyo Machi 29 mwaka huu na wajumbe wake waliapishwa Machi 31. Walipewa siku 20 ya kukamilisha kazi ya kuchunguza kilichoko kwenye makanikia ya shaba maarufu kama mchanga wa dhahabu.
Wajumbe wa kamati hiyo ni Profesa Justianian Rwezaura Ikingula, Profesa Joseph Bushweshaiga, Dk Yusuf Ngenya, Dk Joseph Yoweza Philip, Dk Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.
Kamati hiyo inaongozwa na Profesa Mruma, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) iliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini, ikiwa na makao Dodoma. Mchanga huo wa dhahabu ndio unasafirishwa nje na wachimbaji wa dhahabu wa kampuni ya Acacia ambayo itafunga uzalishaji mgodi wa Buzwagi Desemba 2017.
Licha ya kampuni hiyo pia kuna wachimbaji wadogo ambao wanasafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi ikiwemo Japan kuchenjuliwa na kutenganisha mchanga na madini. Taarifa iliyotolewa jana na kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema Kamati hiyo ya Rais ilikuwa inachunguza mchanga ulio katika makontena ya mchanga wa madini (makinikia) yaliyopo katika maeneo mbalimbali ya migodi hapa nchini.
Tukio hilo litakalorushwa mubashara na baadhi ya vituo vya luninga nchini, litatoa jibu ya maswali ya Watanzania kuhusu kilichomo ndani ya mchanga huo wa dhahabu. Watanzania wengi wanahisi wanaibiwa mchana kweupe kwa maelezo kuwa kampuni zinazofanya biashara hiyo hazina uwazi juu ya kilichomo ndani ya mchanga huo.
Mamlaka za uchunguzi ambazo zilikuwa zinashughulika na ukaguzi wa mchanga huo,TMAA na Mamlaka ya Mapato (TRA) walishatangaza, asilimia 90 ya mchanga ni madini ya shaba, asilimia 0.02 dhahabu na asilimia 0.08 ni fedha. Wakati anawaapisha wajumbe wa kamati hiyo, Rais aliwakabidhi majukumu mazito ya kuingia kila sehemu.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment