CHAMA cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Wilaya ya Bahi katika Mkoa wa Dodoma kimemuomba Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kuingilia kati mgogoro wa uvamizi na uuzwaji kiholela wa maeneo kwa ajili ya malisho katika baadhi ya maeneo wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Bahi katika Kijiji cha Mayamaya Kata ya Zanka, Katibu wa CCWT wilayani Bahi, Dominic Bruno alimwomba Waziri Tizeba kufika katika kijiji hicho ili kutatua mgogoro wa ardhi ya malisho katika Kijiji cha Mayamaya.
Alisema mbuga ya Mayamaya ilitengwa kama malisho tangu mwaka 1972 huku eneo la visima vya maji la Mzigo likitumiwa na wakazi wa vijiji vya Zanka na Mayamaya tangu kuanzishwa kwa vijiji hivyo.
Kwa mujibu wa katibu huyo, kinachowashangaza ni kuona maeneo hayo yameuzwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mayamaya Jonathan Chibalangu kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji huku pia maeneo wanayatumiwa na wafugaji hao kwa malisho ya mifugo yao, nayo yakiwa hatarini kuuzwa.
“Sasa hatuwezi kunyamaza tena tumechoka kuonewa tunamuomba Waziri aje kwani maeneo yetu kwa ajili ya malisho halafu mashamba yanauzwa kiholela tu kwa shinikizo la Mwenyekiti wa kijiji,” alisema.
Mmoja wa wafugaji katika kijiji hicho, Ismail Jumaa alisema jambo linalowauma ni kuuzwa kiholela kwa ardhi katika eneo la Mayamaya kutokana na serikali kutangaza kuwa eneo hilo litakuwa Manispaa ya Dodoma.
“Wanayatamani maeneo yetu tunayoyatumia kwa ajili ya malisho katu hatuwezi kukubali, nasema hivi hatuwezi kukubali tulimwandikia barua Mkuu wa Wilaya aje atatue mgogoro huu,” alisema.
Akitoa ufafanuzi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mayamaya, Jonathan Chibalangu alisema Serikali ya Kijiji cha Mayamaya kwa kushirikiana na ya Kata ya Zanka, wameamua kuunda tume ili kutatua suala hilo.
Alisema awali wanakijiji walifikiri kuwa maeneo hayo yanauzwa na serikali ya kijiji lakini sio kweli, bali wananchi wenyewe ndio wanauza maeneo yao. Aliyataja maeneo yanayogombewa kuwa ni Mbuga za Nzela, Mzigo na Nang’ana’.
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment