Wednesday, April 12, 2017

Serikali yashauri Bunge kujadili utekaji

SERIKALI imelishauri Bunge kukubaliana na hoja ya kuwepo kwa mjadala kuhusu kushamiri kwa vitendo vya utekaji wa viongozi na watu wa kawaida ili kuondoa hofu katika jamii.

Kutokana na ombi hilo, Bunge limelichukua suala hilo ili kulijadili katika vikao vya Kamati ya Uongozi ya Bunge na baadaye kutolea uamuzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alitoa pendekezo hilo kwa Bunge baada ya wabunge kutaka Bunge kuahirisha shughuli zake ili kujadili suala hilo kushika kasi.
Wabunge ambao jana waliomba mwongozo wa Spika wakitaka suala hilo lijadiliwe ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT – Wazalendo).
Aidha, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) na wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) nao walisisitiza umuhimu wa suala hilo kutolewa maelezo ili kuondoa sintofahamu miongoni mwa jamii.
Katika kuonesha kuwa suala hilo linazidi kupamba moto siku hadi siku bungeni, jana Zitto alifika mbali baada ya kuliarifu Bunge kuwa kwa kutumia kifungu namba 120 cha Kanuni za Kudumu za Bunge anajiandaa kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili kuliomba Bunge kuunda Kamati Teule ili kujadili kwa kina suala hilo.
Aliyekuwa wa kwanza kuibua hoja hiyo jana alikuwa Msigwa ambaye aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa kikao cha jana, Mussa Azzan Zungu kuhusu Bunge kukubali kujadili suala hilo ili kulipatia ufumbuzi.
Hata hivyo, kabla ya kiti cha Spika kutoa majibu ya mwongozo huo, Waziri Jenista alisimama na kuomba kiti cha Spika kuangalia uwezekano wa kuruhusu suala hilo kujadiliwa endapo utapatikana ushahidi wa kutosha wa kuwezesha kujadiliwa.
Akitoa msimamo wa kiti cha Spika, Mwenyekiti Zungu alisema suala hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ili kujadiliwa na baadaye (bila kutaja lini) wabunge watataarifiwa uamuzi uliofikiwa.
Pamoja na majibu hayo, wakati wa mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, akichangia Zitto alisema anajiandaa kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili Bunge liunde Kamati Teule ichunguze kwa kina vitendo hivyo vya utekaji kuanzia vilipoanza hadi sasa.
Katika hatua nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelaani vitendo hivyo vya utekaji watu, ikisema vinaashiria kuwepo kwa makundi yanayoendesha matendo ya utekaji watu kinyume cha sheria.
“Matukio ya hivi karibuni ya kuvamia kampuni za tasnia ya habari na mawasiliano au kuwateka watu, yanaashiria kutoweka kwa uvumilivu wa uwepo wa maoni tofauti katika jamii kuhusu mambo mbalimbali,” ilieleza taarifa ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga.
“Tume inapenda kusisitiza kwamba katika nchi yenye demokrasia, serikali ina wajibu na jukumu la kuzilinda haki hizi, na pia kuwalinda wananchi dhidi ya matendo yanayodhalilisha utu wao, utesaji, na matendo yote yanayowanyima uhuru na haki zao za msingi, ikiwemo haki ya maoni na uhuru wa kujieleza,” alieleza Nyanduga.
Tume imeshauri vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, vifanye uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo, na kuchukua hatua zipasazo za kisheria kuhakikisha waliohusika na kupotea kwa Bernard Saanane, na utekaji wa Salma Saidi, Ibrahim Mussa (Roma Mkatoliki) na wenzake wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment