Tuesday, April 18, 2017

Serikali kuanzisha ‘Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa’

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iko katika mchakato wa kuanzisha ‘Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa’ ambao una dhima kubwa ya kusaidia kuinua kipato.

Naibu Waziri wa Wizara Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura
Aidha mfuko huo utaongeza tija na weledi kupitia utaratibu wa upatikanaji fedha utakaowekwa ili kuwawezesha wasanii kuzalisha kazi bora za sanaa zenye kukidhi viwango vya masoko ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Maulid Said Mtulia aliyeuliza juu ya mpango wa serikali kuwaongezea vifaa, mitaji na menejimenti vijana walioamua kujiajiri katika sanaa mbalimbali kama vile maigizo, maonesho ya mitindo na michezo mbalimbali, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Annastazia Wambura alisema serikali yake ipo katika harakati za kuwajengea vijana mazingira mazuri ya kufanya shughuli za sanaa.
Vilevile Naibu Waziri Wambura, ameeleza kuwa katika kipindi ambacho mfuko wa maendeleo ya sanaa unaandaliwa, Serikali inashauri Halmashauri zote ziwasaidie vijana wanaojishughulisha na sanaa kwa kuwapa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa ajili ya mitaji kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato ya kila Halmashauri kwa kuwa sanaa ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana kwa sasa.


source:bongo5
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment