Tuesday, April 11, 2017

Mvua yaharibu nyumba 100

NYUMBA zaidi ya 100 kwenye kata ya Bwiringu na baadhi katika kata ya Msoga zimeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Pwani na kuwafanya baadhi ya wananchi kujihifadhi kwa majirani zao.
Mvua hizo zilizonyesha mwishoni mwa wiki ziliambatana na maji mengi ambayo yalibomoa nyumba hizo kabisa na baadhi ya vitu kusombwa na maji.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga alisema hadi sasa baadhi ya kaya zinaishi kwa majirani kutokana na nyumba zao kubomoka kabisa na hazifai kukaliwa.
Mwanga alisema maji hayo yalifika usawa wa madirisha na baadhi ya vitu vilisombwa na maji na havikupatikana huku baadhi ya nyumba zikianguka.
“Tumefika hapa kuona uharibifu uliosababishwa na mvua hizi ambazo bado zinaendelea kunyesha, serikali inafanya tathmini kujua uharibifu uliofanyika na kujua idadi kamili ya watu walipata athari hizo,” alisema Mwanga.
Alisema hadi sasa hakuna taarifa ya mtu kupoteza maisha zaidi ya mali, mazao na nyumba kuharibiwa na mvua hizo zinazonyesha kwa wingi ambazo hazijawahi kutokea kwa kipindi kirefu hadi kuleta madhara kama hayo.
“Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia wenzetu ambao wamekumbwa na madhara haya kwani wanahitaji misaada mbalimbali ya kibinadamu,” alisema Mwanga.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bwiringu, Lucas Lufunga alisema athari ya mvua hizo ni kubwa sana na si mvua za kawaida kwani miaka mingine mvua zinakuwa nyingi lakini hazina madhara kama haya.
Lufunga alisema tayari wamewasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri kwa ajili ya kuangalia nini cha kufanya kwa wananchi hao.
Naye mkazi wa Chalinze Mzee, Said Abdala alisema mvua hizo zilianza alasiri, lakini ilipofika usiku maji mengi yalianza kuingia kwenye nyumba zetu na kutuletea madhara haya.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee, Cecilia George alisema mvua hizo zimemletea athari kwani vifaa vyake vya shule yakiwemo madaftari na vitabu pamoja na sare zake vimebebwa na maji.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.


0 comments:

Post a Comment