Saturday, April 8, 2017

Kifusi chaua, chajeruhi, wengine wawili watafutwa

MTU mmoja amekufa na mwingine kuvunjika mguu huku wawili wakiendelea kutafutwa baada ya kufunikiwa na kifusi katika machimbo ya kokoto yaliyopo eneo la Golani, Pugu Kigogo Freshi, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nane mchana huku chanzo kikiwa ni kuporomoka kwa udongo katika eneo hilo.
Alisema baada ya tukio hilo kutokea waliwasiliana na Polisi kwa ajili ya kufanya uokoaji ambapo walifanikiwa kuwatoa watu wawili ambapo mmoja alitoka akiwa amevunjika na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana na mwingine akiwa amekufa na mwili wake kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha lakini tunaendelea na jitihada za kuwaokoa waliobaki ndani ya kifusi, Aprili 6 tulisitiza shughuli ya uokoaji baada ya kuona udongo ukiwa unaendelea kuporomoka kila baada ya dakika ishirini tukaona tusitishe kwasababu haikuwa salama, sasa hivi tunasubiri tupate ‘escaveter’ na wataalamu ambao wataona ni jinsi gani wataweza kuwaokoa wale waliobaki,”alisema Mjema.
Aliongeza kuwa eneo hilo sio rasmi kwa ajili ya uchimbaji wa kokoto kwa kuwa tayari serikali ililifungia miaka miwili iliyopita lakini watu hao waliendelea kufanya shughuli zao kwa kujiiba.
“Tumeshindwa kuelewa ni kwa nini watu hawa waliendelea kufanya shughuli zao wakati tayari tulifunga eneo hili, tumepata taarifa kuwa kuna mtu anadai eneo hili ni mali yake na alikuwa akiwaruhusu watu kuingia kisha anawatoza fedha kwahiyo tutamtafuta na wale wote waliokuwa wakirusu eneo hili kuendelea kufanya kazi tutawatafuta na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,”aliongeza Mjema.
Mjema alisema sio mara ya kwanza kutokea kwa ajali kama hiyo kwani miaka miwili iliyopita ilitokea na kusababisha vifo vya watu kadhaa na Mkuu wa Mkoa wa wakati huo, Said Meck Sadick aliamua kufunga machimbo hayo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Ilala, Ully Mbuluko alisema, wanaendelea na jitihada za uokoaji ambapo wanasubiri gari maalumu la uokoaji ili kuona namna ya kuwafikia waliopo ndani.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi na kuwataka kuacha kuendelea na shughuli katika eneo hilo kwakuwa tayari serikali walishalifunga miaka miwili iliyopita ili kujiepusha na madhara yanayoweza kutokea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni alikiri kutokea kwa tukio hilo na aliwataja waliokuwa wamefukiwa kuwa ni Rashid Fadhil (28), Amos Debwa (27)ambaye ametolewa akiwa amekufa, Boniface Pius (30) na Shabani Omary (27) ambaye amevunjika mguu.
Alisema wanaendelea kushirikiana na idara mbalimbali za Serikali ikiwemo Manispaa ya Ilala kuhakikisha miili hiyo inaokolewa na inakwenda kuzikwa.
Hamduni alisema ili kudhibiti madhara mengine yasitokee jeshi hilo litaweka ulinzi katika eneo hilo na yeyote atakaeingia katika eneo hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Gazeti hili lilipata fursa ya kuzungumza na baadhi mashuhuda wa tukio hilo, Mohamed Seleman ambaye ni mmoja wa vijana wanaofanya shughuli zao katika machimbo hayo alisema siku ya tukio hilo alitaka kufanya kazi lakini moyo wake ulisita akaamua kuondoka lakini baada ya muda alirejea na kushuhudia wenzake wakifukiwa.
“Tulikwenda kunywa chai pamoja lakini siku hiyo moyo wangu ulisita kufanya kazi nikaamua kuondoka lakini wakati narudi ndio tukio likaanza kutokea tuliamua kuwaokoa wenzetu na kufanikiwa kumtoa mmoja akiwa amevunjika mguu wakati akijaribu kuruka,”alisema.
Alisema baada ya jitihada zao kushindwa waliamua kupiga simu Serikali za Mitaa na walifika lakini waliona vifaa vinavyotumika kuokoa havitaweza kufanya kazi hiyo hivyo walilazimika kuomba nguvu zaidi kutoka Manipsaa ya Ilala na kufanikiwa.
Aidha, wananchi waliokuwepo kushuhudia tukio hilo walikiri kuzuiwa kuendelea na shughuli katika eneo hilo lakini hali mbaya ya maisha iliwafanya kuendelea.
Walisema kama serikali iliamua kuzuia machimbo hayo ilipaswa kurudi mara kwa mara ili kuangalia kama shughuli zinaendelea au la.
Gazeti hili pia lilifanya jitihada ya kufika katika Hospitali ya Amana ili kumuona Omary ambaye Mkuu wa Wilaya alidai alipelekwa katika Hospitali hiyo.
Ofisa Muuguzi wa zamu Getrude Massawe alikiri kumpokea Omary majira ya saa kumi jioni akiwa amevunjika mguu wa kulia lakini alihudumiwa na kuruhusiwa kuondoka kwa kuwa hakuwa katika hali mbaya.

Source:millardayo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment