Friday, March 31, 2017

Waajiriwa Afya 192 kwa ufadhili wa CDC waitwa

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewaita watu 192 waliofaulu usaili wa ajira za dharura kupitia ufadhili wa Kituo cha Kuzuia na Kusimamia Magonjwa (CDC) kufika wizarani Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Watu hao ni matabibu wasaidizi na wauguzi waliopata ajira hiyo ya mkataba wa miezi 16 kwa lengo la kukabiliana na uhaba mkubwa wa wafanyakazi katika sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubya alisema hayo kwenye taarifa aliyoitoa ya kuwataka watu hao kufika wizarani Jumanne ijayo kwa ajili ya kujaza mikataba na kupangiwa vituo vya kazi.
Dk Ulisubya aliwataka watu hao kufika siku hiyo saa tatu asubuhi kwa ajili ya kujaza mikataba na kupangiwa vituo vya kazi.
Ajira hizo za dharura ni msaada uliotolewa na taasisi hiyo ya Kimarekani ya CDC kwa ajili ya kuwawezesha watu hao kufanya kazi hizo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akifafanua hilo, Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja alisema watu hao hawataingia kwenye mfumo rasmi wa ajira, bali wamechukuliwa kwa mkataba maalumu kutokana na fedha hizo za wahisani.
Nafasi hizo 192 zilitangazwa mwaka jana na wizara hiyo kwa wataalamu wa fani mbili za afya ambazo ni tabibu wasaidizi nafasi 95 na wauguzi nafasi 97, mpango ambao utaendeshwa kwa miaka miwili.
Watumishi hao waliochaguliwa watapangiwa vituo vya kazi vilivyoko katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa watumishi husika na ambayo mazingira yake ni magumu, na kwamba baada ya kumaliza mkataba wao, wataingizwa katika ajira za serikali kulingana na upatikanaji wa vibali vya ajira kwa mwaka husika.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment