Tuesday, March 28, 2017

Mwigulu:Polisi acheni kufukuzana na bodaboda

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewataka askari Polisi nchini kuacha tabia ya kufukuzana na waendesha bodaboda, kwani mara nyingi tabia hiyo imekuwa ikisababisha ajali.

Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuacha tabia ya kubambikia wananchi kesi, kuwabadilishia mashitaka na kuacha kutumia taarifa pekee za watu wanaohasimiana kuwa chanzo cha mashitaka.
Akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Maofisa Waandamizi wa Polisi mjini hapa, Mwigulu alitaka kuwepo kwa mbinu za ukamataji wa waendesha pikipiki hao, kwani tabia ya kuwakamata kwa kuwakimbiza mara nyingi imekuwa ikisababisha ajali.
Mwigulu alisema kumekuwa na changamoto kubwa za ajali za pikipiki na ukubwa wa tatizo hilo unaweza kuonekana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambayo imeelemewa na wagonjwa na kinachotakiwa kufanyika ni kutolewa kwa elimu.
Alisema ipo haja ya kutengeneza mtandao wa kujua vijana kwa kila eneo na watambue dhamana waliyonayo ni kubwa na elimu lazima iwafikie.
Alisema kumekuwa na ajali zaidi ya 7,000 kwa mwaka ambazo zinasababisha vifo zaidi ya 2,000.
“Huwezi kusema idadi ya wanaokufa ni ndogo kwa vile ni bodaboda,” aliongeza na kulitaka jeshi hilo kuendelea kuchapa kazi na kupanga mikakati mipya ya kuzuia na kupambana na uhalifu nchini.
“Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kama hakuna amani na usalama wawekezaji hawawezi kuwekeza mahali ambapo hakuna mazingira salama,” alisema Mwigulu na kuongeza kumekuwa na tabia ya askari kubambikia watu kesi na kubadilisha kesi hasa kwa wale wanaoshindwa kutoa rushwa.
Alisema hilo ni jambo lisilopendeza kwa Polisi na kuwataka kuacha hata kutumia taarifa pekee za watu wanaohasimiana kuwa chanzo cha mashitaka, kwani jambo hilo limekuwa halitendi haki.
Aliwataka kutumia weledi katika kufanyia uchambuzi ili mwenye makosa afikishwe kwenye mikono ya sheria na asiye na kosa aachiwe aendelee na shughuli zake.
“Kuna malalamiko kwa maofisa wa Polisi kubambikia watu kesi hasa pale wanapokataa au kushindwa kutoa rushwa, sisi tupo kwa ajili ya wanaoonewa kuona wanyonge wanapata haki zao lazima tuepuke suala la ubambikiaji wa kesi,” alieleza.
Aliwataka kuwa na mbinu mbadala za kupambana na uhalifu na kila mkoa ujitahidi kupambana na dawa za kulevya.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya operesheni ili kuwabaini wanaouza na kusambaza dawa za kulevya, akibainisha kwamba kumekuwa na tatizo kubwa nchini la ulimaji wa bangi katika mikoa mingi na wataendelea kufyeka mashamba hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu alisema kamati hiyo inaelewa matatizo ya Jeshi la Polisi na watahakikisha wanapata bajeti nzuri.
Alisema serikali inategemea sana polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama, na aliwataka kupambana na dawa za kulevya.
Pia alisema makamanda wa polisi wana jukumu la kuwarekebisha viongozi wao wa mikoa pale wanapokwenda kinyume na wasisubiri hadi mambo yaharibike.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment