Wednesday, March 29, 2017

Mchanga wa dhahabu Buzwagi kupelekwa kwa mkemia mkuu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amechukua sampuli ya mchanga wa dhahabu kwa ajili ya kuupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili aupime na kuona kuna aina ngapi na kiasi gani cha madini kinachopatikana kwenye michanga hiyo.
Pamoja na hayo, ameitaka Kampuni ya Acacia inayomiliki migodi miwili ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu kuwekeza kwa kujenga kiwanda cha uchenjuaji wa dhahabu hapa nchini kama walivyokubaliana na serikali kabla ya kuanza shughuli zao za uchimbaji wa madini ya dhahabu nchini.
Alisema kwa sasa lazima migodi iwe wazi kwa shughuli wanazozifanya ili Watanzania wengi wajue nini kinafanyika na kuondoa fikra potofu baina yao ya kuwa wawekezaji hao wamekuwa wakiiba malighafi ya nchi na kupeleka kwao kwa lengo la kujinufaisha huku taifa likibaki bila kitu.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alipata fursa ya kuangalia makontena zaidi ya 180 yaliyokuwepo katika mgodi huo huku akifungua baadhi ya makontena ili achukue sampuli za mchanga huo wa dhahabu na kwenda kuupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuona ni kiasi gani cha madini yaliyopo katika mchanga huo.
Aidha, aliwataka wawekezaji wa kampuni hiyo kupitia migodi yake miwili ya Buzwagi na Bulyanhulu kutowapunguza kazi watumishi wake kutokana na kauli ya Rais John Magufuli kuzuia usafirishwaji wa makontena ya mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji.
Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa serikali ipo pamoja nao na kuongeza kuwa juu ya suala la kusafirisha makontena hayo kwenda nchi za nje kutakuwa na mazungumzo baina ya pande hizo zote mbili na kuongeza kuwa lazima muafaka utapatikana katika siku za baadaye.
Alisema kwa sasa serikali itakaa na wawekezaji hao kuona mchakato wa jinsi wao wanaweza kujenga mtambo wa uchenjuaji wa madini hayo na kuondoa maneno kwa Watanzania ya kuwa madini hayo yamekuwa yakiibwa kupitia mchanga unasafirishwa nchi za nje kwa ajili ya uchenjuaji.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Madini kutoka Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), Eradius Erasto alisema hadi sasa kuna jumla ya makontena 180 ya mchanga wa dhahabu yapo katika mgodi huo, 21 yakiwa tayari yapo bandarini wakati 152 yakiwa yapo katika Kampuni ya Zamcargo ya jijini Dar es Salaam.
Naye Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi, Stewart Hamilton alisema wao kama kampuni wanasubiri uamuzi utakaotolewa baina ya mazungumzo ya pande hizo mbili na kubainisha kuwa anatarajia kuafaka utafikiwa.

Source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment