Wednesday, March 15, 2017

Makonda aagiza bomoabomoa Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kubomolewa kwa nyumba 36, ambazo zipo kwenye maeneo hatarishi ya mabondeni, ikiwemo bonde la Mto Msimbazi wilayani Ilala kuanzia leo.
Pia amewataka wananchi wa maeneo hayo, ambayo tayari wamepewa viwanja katika eneo la Mabwepande kwenda katika maeneo yao.
Makonda alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea nyumba hizo katika eneo la Mto Msimbazi, Buguruni kwa Mnyamani na Tabata, akiwa na vikosi vya ulinzi na usalama, ambako ameshuhudia maafa makubwa yakiwemo ya baadhi ya watu kupoteza mali pamoja na nyumba zao kujaa maji.
Alisema anataka shughuli hiyo ya ubomoaji, ianze leo kwa kuwa tayari watu hao wameshalipwa na walipaswa kuondoka katika nyumba hizo.
Aidha, aliwataka wananchi ambao hawajafidiwa wafike katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ili kukamilisha utaratibu wa fidia zao.
“Eneo hili la Msimbazi tayari tumewapoteza watu, hatutaki kuendelea kupoteza watu wengine, haya sio maeneo salama ya kuishi. Nahitaji kuona kazi ya ubomoaji ikianza kesho (leo) kama hujapata fidia fika katika ofisi ya Mkurugenzi. nataka kuona mwezi wa nne eneo hili likiwa wazi,” alieleza Makonda.
Aidha, Makonda alisema amepata taarifa kuwa kuna watu waliopewa viwanja Mabwepande katika Manispaa ya Kinondoni, lakini wameamua kuweka wapangaji katika nyumba zao zilizopo katika maeneo hayo hivyo amewataka watu wote waliopanga katika nyumba hizo kuondoka.
“Hivi wewe hujiulizi ni kwa nini mtu huyu kahama katika nyumba yake anakupangisha na wewe unakubali wakati unajua kabisa eneo hilo sio salama, naomba muondoke hatutaki kutumia nguvu,” aliongeza Makonda.
Mvua za masika zilizoanza kunyesha kuanzia Machi 8, mwaka huu, zimesababisha maafa ikiwemo vifo pamoja na wananchi wengi wa mabondeni kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kujaa maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Hii si mara ya kwanza kwa mkoa huo, kuwaondoa wanaoishi mabondeni.
Kila mwaka wamekuwa wakiondolewa na wengine kurejea tena kinyemela. Wengine hawajawahi kuhama Msimbazi, licha ya maafa yanayotokea kila mwaka.

0 comments:

Post a Comment