Thursday, February 9, 2017

Sheikh aunga mkono juhudi za Makonda kupambana na dawa za kulevya

Baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya Tanzania linaunga mkono juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kupambana na dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam Jumatano hii, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum ,alisema Makonda anapaswa kuongezewa ulinzi kutokana na ujasiri aliouonesha wa kuthubutu kuwataja kwa majina watu hao.”Tunampongeza kwa dhati kabisa mkuu wa mkoa kwa ujasiri aliouonyesha kwa kuwa ameamua kujitoa mhanga kwa ajili ya Taifa,”amesema.
“Sisi kama baraza tunapinga vita na kulaani hatua yoyote ya kushiriki katika biashara au utumiaji wa dawa za kulevya kwakuwa matumizi ya dawa hizo yamekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika nchi yetu na yanapoteza nguvu kazi ya Taifa kwa vile wahanga wakubwa wa matumizi ya dawa hizi ni vijana,” ameongeza Sheikh Salum.
Hata hivyo amesema kutokana na ugumu wa kazi hiyo aliyoianzisha baraza hilo linamuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ampe ulinzi wake na kinga yake na azidi kumpa moyo wa ujasiri wa kupambana na maovu yote yanayoharibu sifa ya Taifa na vijana kwa ujumla.
Aidha sheikh huyo amesema inawezekana wanaopinga au kubeza juhudi hizo ni kwa sababu tu madhara ya dawa za kulevya hayajawagusa wao na familia zao hivyo hawana uchungu na watanzania wenzao walioathirika hivyo wapuuzwe badala yake wasimame pamoja kama watanzania dhidi ya vita hiyo.
By: Emmy Mwaipopo


0 comments:

Post a Comment