Monday, February 20, 2017

Mugabe- Sioni wa kunirithi

RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe kesho anatimiza umri wa miaka 93. Mwanasiasa huyo amesema hana mpango wa kuachia madaraka kwa sababu mpaka sasa hana mrithi anayekubalika kuvaa viatu vyake.

“Kutakiwa kuachia madaraka lazima niambiwe na kamati kuu ya chama changu na chama changu bungeni,” alisema Mugabe wakati akihojiwa na kituo cha redio na taarifa hizo kuchapishwa kwenye gazeti la serikali la Sunday Mail.
“Lakini kinachoonekana ni nini? Ni kinyume. Wananitaka nigombee tena kwenye uchaguzi mkuu, watu wengi wanahisi hakuna anayestahili kunirithi kushika nafasi yangu” amesema.
Mugabe alianza kuiongoza Zimbabwe mwaka 1980 akiwa Waziri Mkuu hadi mwaka 1987 alipochaguliwa kuwa Rais.
Hivi karibuni mkewe,Grace aliuambia umma wa Zimbabwe kuwa kwa sababu ya umaarufu wa mumewe, hata akiaga dunia Wazimbabwe wataichagua maiti yake iwe Rais.
Mugabe amewahi kusema kuwa, hataondoka madarakani hadi Mungu atakapomchukua.


0 comments:

Post a Comment