Na Baraka Mbolembole
SIMBA SC walipokea kipigo cha tatu msimu huu siku ya Jumamosi iliyopita na mabingwa watetezi Yanga SC walifanikiwa kupata ushindi wa 14 katika ligi kuu Tanzania bara na kurejea kileleni mwa msimamo kwa alama moja zaidi ya Simba huku ikisalia michezo kumi kabla ya ligi kumalizika kwa msimu.
Kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam FC kimeiporomosha Simba kutoka katika kilele cha msimamo na sababu kubwa ya kuporomoka kwa kikosi hicho cha kocha Mcameroon, Joseph Omog na msaidizi wake Mganda, Jackson Mayanja ni timu kushindwa kufunga magoli ya kutosha.
Wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi Disemba 2016 niliandika makala na kusema ili Simba waendelee ‘kubahatisha’ kushinda ubingwa msimu huu walipaswa kumsaini mshambulizi wa Mtibwa Sugar, Rashid Mandawa ambaye alifunga magoli 7 katika michezo ya mzunguko wa kwanza akiwa na ‘Wakata Miwa’ hao wa Turiani, Morogoro.
Lakini uongozi wa timu hiyo uliamua vingine na kuwasaini wachezaji wanne-golikipa Mghana, Daniel Agyei, kiungo wa kati raia wa Ghana, James Kotei, kiungo wa mashambulizi, Pastory Athanas kutoka Stand United na mshambulizi Mtanzania, Juma Ndanda Liuzio ambaye yeye amesajiliwa kwa mkopo akitokea Zesco United ya Zambia.
Baada ya usajili huu nilisema wazi ‘hakuna kipya’ kitakachoongezwa na wachezaji hao na kinachoendelea sasa ni kielelezo kuwa usajili wa timu hiyo haukuzingatia mapungufu muhimu yaliyokuwepo kikosini huku baadhi ya viongozi wakihusika katika sajili hizo na si makocha.
Je, ni kweli Simba iliwahitaji Liuzio, Pastory na Kotei? Upande wao walifaa, lakini nilihitaji kuona timu hiyo ikijiimarisha zaidi katika ufungaji na mtu pekee ambaye alikuwa na nafasi ya kuingia moja kwa moja na kufanya vizuri ni Mandawa ambaye licha ya uwezo wake mzuri katika umiliki wa mpira, mshambulizi huyo ana nguvu na uwezo wa kufunga.
Liuzio hakuwa katika kiwango kizuri kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa ametoka katika majeraha yaliyokuwa yakimsumbua kiasi cha kupoteza nafasi yake katika timu ya Zesco. Pastory licha ya kufunga magoli mawili akiwa Stand United kijana huyo si mfungaji wa kutegemewa lakini ni mchezaji ambaye anaweza kucheza vizuri kama kiungo wa mashambulizi ndiyo maana alifanikiwa kupiga pasi 7 zilizozaa magoli akiwa Stand.
Kotei sijui kwanini alisajiliwa kwa sababu tayari Omog alikuwa ana hazina kubwa ya wachezaji wa nafasi ya kiungo. Usajili wa Agyei kwangu niliuhitaji kutokana na golikipa aliyekuwepo awali Muivory Coast, Vicent Aghban kutokuwa makini katika uchezaji wa mipira ya wazi huku tabia yake ya kucheza mbali na goli ilikuwa haipendezi.
MECHI TANO MAGOLI MANNE
Hakuna mshambuliaji aliyefunga goli katika kikosi cha Omog tangu kuanza kwa mzunguko wa pili ambao wamekwisha kucheza michezo mitano. Walishinda 2-0 ugenini vs Ndanda FC kwa msaada wa magoli ya viungo, Muzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim.
Wakashinda 1-0 dhidi JKT Ruvu, wakapata tena ushindi ‘kiduchu’ wa 1-0 vs Ruvu Shooting, kisha wakalazimisha suluhu-tasa ugenini dhidi ya Mtibwa kabla ya kupoteza 1-0 mbele ya Azam FC wikendi iliyopita.
Katika michezo yote hii mitano hakuna mshambuliaji aliyefanikiwa kufunga jambo ambalo kwa timu inayohitaji ubingwa wa ligi ni tatizo kubwa. Huwezi kushinda ubingwa ikiwa washambuaji wako hawafungi magoli.
Na tatizo hili japokuwa linaweza kumuhusu kocha Omog na msaidizi wake Mayanja lakini kwa kiasi kikubwa limesababishwa na uongozi wa timu ambao uliwahitaji wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo badala ya kumuachia kocha jukumu la usajili. Omog alimuhitaji Mandawa lakini uongozi ukaleta sababu za kimaslai na kushindwa kumsaini mfungaji huyo mwenye uzoefu wa ligi kuu Bara.
HAKUNA UBINGWA KWA SIMBA 2016/17
Tangu mwanzo wa msimu nimekuwa nikiamini Simba haina kikosi kilichokomaa ili kushinda ubingwa wa kwanza wa VPL tangu msimu wa 2011/12. Ukomavu ninaouzungumzia ni ule wa wachezaji kulinda viwango vyao kwa muda mrefu.
Shiza Kichuya ambaye alifunga magoli 9 katika michezo ya mzunguko wa kwanza alitumia nguvu nyingi, akili lakini sasa kuelekea michezo kumi ya mwisho mchezaji huyo ameshuka kiwango. Aliingia kuchukua nafasi ya Jamal Mnyate katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC na kitendo cha kuwekwa benchi katika mchezo huo muhimu ni ishara kwamba kiungo huyo mshambulizi wa pembeni yupo ‘katika maji marefu’ hivi sasa.
Kabla ya kuwavaa Azam walinzi Method Mwanjale na Abdi Banda walikuwa na matatizo lakini wakajikaza na kucheza mchezo huo kwa sababu timu haikuwa na machaguo mbadala. Kiungo Mohamed Ibrahim ambaye amefunga magoli manne anauguza majeraha aliyopata katika michezo ya Mapinduzi Cup huko Zanzibar.
Kukosekana kwake ni pengo kubwa katika mipango ya Omog kutokana na kwamba mchezaji huyo hutengeneza nafasi nyingi za kufunga pia hufunga katika mazingira yasiyotarajiwa na wengi. Muzamiru, nahodha Jonas Mkude, Kichuya na Mohamed Ibrahim walishatengeneza safu nzuri ya kiungo lakini sasa mambo yamekuwa magumu.
Kutoka mbele ya pointi nane dhidi ya Yanga hadi kuwa nyuma kwa alama moja zikiwa zimesalia mechi kumi kabla ya kumalizika kwa msimu ni dalili mbaya, lakini hili nilitaraji kutokana na aina ya wachezaji waliopo Simba hivi sasa. Wana nia hasa ya kushinda ubingwa lakini hawawezi kufikia lengo hilo kutokana na kwamba hakuna yeyote klabuni hapo anayejua jinsi ya kushinda ubingwa huo.
Pointi tatu katika michezo yao mitano ijayo yatakuwa mafanikio kwa sababu hawana uwezo wa kufunga magoli na wachezaji walijivika majukumu ya ufungaji (Kichuya, Muzamiri na Mohamed Ibrahim) wanaanza kuyumba. Simba walizidiwa kufunga tu na Azam FC ndiyo maana wakapoteza mchezo huo.
Wikendi ijayo watakuwa Songea kucheza na Majimaji FC, kisha wataivaa Yanga, Tanzania Prisons, Mbeya City FC na kusafiri Kanda ya Ziwa kucheza michezo mitatu migumu dhidi ya Kagera Sugar, Mbao FC na Toto Africans. Katika michezo hii mitano ijayo ya Simba wanaweza kupata alama 6 kama watagangamala, na huenda pia wasipate pointi hizo na kuambulia 3 tu.
Si rahisi Simba kuondoka na pointi 3 katika michezo mitatu ya Kanda ya Ziwa na uwezo wa Majimaji na Yanga ni kielelezo kuwa wapo karibu kupoteza kabisa matumaini yao ya ubingwa ambao waliamini wanaweza kutwaa mwanzoni mwa msimu.
Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib kiujumla wamefunga magoli 7 katika VPL msimu huu-sawa na magoli yaliyofungwa na Obrey Chirwa pekee katika kikosi cha Yanga. Ili mambo yaende vile wanavyotaka Omog na Mayanja huu ni wakati wao wa kuwekeza mbinu mpya za ufungaji vinginevyo wataondolewa.
Simba SC itashinda VPL msimu huu? Angekuwepo Hamis Kiiza katika kikosi chao cha sasa wangeshinda lakini uwepo wa Mavugo, Ajib, Liuzio, Pastory kama wafungaji tegemewa ni ndoto kufikia matarajio yao hayo.
Simba haiwezi kushinda ubingwa kwa kutegemea kikosi hiki walichonacho sasa, ila watakuja kushinda misimu ijayo wakati ambao utawala utajua umuhimu wa timu kusajiliwa na kocha.
0 comments:
Post a Comment