WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kushuhudia wazee wa kimila wakipooza ardhi na kuomba dua ya amani na maridhiano kuhitimisha uhasama uliokuwepo kati ya wakulima na wafugaji kwa miaka mingi wilayani Kiteto mkoani Manyara ambao uliambatana na mauaji.
Hatua inatokana na Waziri Mkuu, Majaliwa kutarajiwa ziara ya kikazi ya siku sita mkoani Manyara kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi, kuzungumza na watumishi wa umma waliopo katika mkoa huo pamoja na kuzungumza na wananchi katika mikutano mbalimbali ya hadhara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alisema ziara hiyo inatarajiwa kuanza kesho hadi Februari 20, mwaka huu ambayo pamoja na mambo mengine, atashuhudia sala hiyo maalumu ya kuombea amani katika maridhiano ya kuhitimisha uhasama uliokuwepo Kiteto kati ya wafugaji na wakulima.
Dk Bendera alisema Waziri Mkuu akiambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa atawasili kesho saa tatu asubuhi wilayani Kiteto ambako atalakiwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo, katibu tawala pamoja Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mkoa.
Alisema akiwa wilayani Kiteto ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa ofisi za halmashauri ya wilaya hiyo na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye uwanja wa michezo uliopo mjini Kibaya.
Alifafanua kuwa Februari 16, Waziri Mkuu atafanya ziara wilayani Simanjiro ambako atapokea taarifa ya wilaya na kuzungumza na watumishi wa umma kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo ambako pia atasalimiana na wananchi wa mji wa Orkesmert na kukagua mradi wa upimaji wa viwanja na kuona mradi wa barabara ya KIA –Mirerani.
Aidha, alieleza kuwa Februari 17, mwaka huu, Waziri Mkuu atakuwa wilayani Mbulu ambako atatembelea Hospitali ya Rufaa ya Haydom ambako atapokea taarifa fupi ya hospitali hiyo na kuzungumza na watumishi wa umma wa Wilaya ya Mbulu, wananchi wa mji wa Mbulu kwenye Uwanja wa Getini.
Ratiba ya ziara hiyo inaonesha kuwa Waziri Mkuu atakuwa wilayani Hanang’, Februari 18, ambako atapokea taarifa ya wilaya na kuzungumza na watumishi wa umma na kuzindua majengo ya madarasa ya Shule ya Msingi Mogitu na atazungumza na wananchi wa Mji wa Katesh kupitia mkutano wa hadhara Uwanja wa Shule ya Msingi Katesh.
Aidha, akiwa wilayani Babati, Jumapili wiki hii atapokea taarifa ya wilaya, kuzungumza na watumishi wa umma, atakagua mradi wa maji Minjingu, atakagua Kiwanda cha mbolea Minjingu, ataweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa daraja la Bonga –Endanachani na kuzungumza na wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Kwaraa.
Jumatatu ijayo, Waziri Mkuu atafanya majumuisho ya siku sita ya ziara yake mkoani Manyara katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambako Mkuu wa mkoa huyo aliwataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumpokea kwa kuwa kiongozi wa kitaifa husaidia kushauri na kusukuma maendeleo ya mkoa.
0 comments:
Post a Comment