Monday, February 13, 2017

JPM: Hata Waziri Mkuu Hakulijua Hili..!!!

Rais John Magufuli amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  alikuwa hajui kama yeye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kudhibiti Dawa za Kulevya kama ilivyobainishwa kwenye sheria.

Rais Magufuli amesema hayo wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali, Ikulu na kuagiza wakachape kazi bila kumuogopa mtu yeyote.

“Kama anajua, amejua jana au leo. Nina uhakika hata mawaziri wake ambao ni wajumbe wa baraza hilo walikuwa hawana taarifa na hakuna aliyewakumbusha,” amesema Rais na kuongeza: “Hata mimi sikuletewa mapendekezo ya kumteua kamishna mkuu wa mamlaka hii (ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga). Nilimteua kwa sequence (utaratibu) niliyonayo mwenyewe. Lazima tuwe wa kweli, tusijifanye malaika kwa kuficha ukweli,” alisema Rais Magufuli.

Pia, ameeleza kuchukizwa na kitendo cha watu kwenda Kituo Kikuu Polisi (Central) na kuanza kuosha gari la mtuhumiwa huku wengine wakienda na kwaya katika eneo hilo.

Tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita wakati mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji alipokwenda kuripoti polisi na baadhi ya mashabiki wake kuosha gari lake lililokuwa limeegeshwa katika kituo hicho.

Wengine wanaoaminika kuwa ni wanakwaya wa Kanisa la Ufufuo na uzima linaloongozwa Askofu Josephat Gwajima walifika eneo hilo wakati kiongozi wao alipokwenda kuhojiwa huku wakiimba nyimbo mbalimbali.


“Sitaki kuona tena wananchi wanajazana kituo cha polisi watuhumiwa wanapohojiwa. Lazima tujenge nidhamu, mbona hawakwenda Lugalo kwa CDF (Mkuu wa Majeshi) kuimba kwaya?” amesema Rais Magufuli huku akimuagiza Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro.


0 comments:

Post a Comment