Tuesday, January 17, 2017

Vyama Burundi vyamuomba Mkapa asizungumze

BAADHI ya viongozi wa vyama vya siasa nchini Burundi wanaoshiriki vikao vya usuluhishi jijini Arusha wamemuomba msuluhishi wa mgogoro wa kisasa nchini Burundi, Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutokuwa mzungumzaji katika kikao hicho, bali awe msikilizaji zaidi.

Hayo wameyasema jana jijini Arusha wakati wakitoa maoni wakati wa kikao cha siku moja kwa ajili ya kujadili hatma ya amani nchini Burundi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa AICC jana, mmoja kati ya wajumbe wa mkutano huo, Bigirimana Jacquees alisema hawapingani na msuluhishi wa mgogoro huo ambaye ni Rais Mkapa, bali wanachotaka ni kutokuwa mzungumzaji zaidi katika kikao hicho.
Amesema wao wanataka wazungumze wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia lugha zao na kunyoosheana vidole, badala ya msuluhishi huyo kuwa mzungumzaji zaidi.
“Tunataka amani katika nchi yetu na hatutaki migogoro baina yetu na Warundi wakisikia tumemkataa msuluhishi wetu wanahuzunika sana, lakini tunachomuomba atupe nafasi ya kuzungumza sisi wenyewe kwa wenyewe badala ya yeye kuzungumza sana,” alisema Jacquees.
Awali mmoja kati ya mawakili wa kujitegemea kutoka Burundi, Ali Mbongo amesema Warundi wanahitaji amani ikiwemo Kiswahili kupewa kipaumbele kwani pia katika nchi hiyo kuna kabila la Waswahili ingawa halipewi nafasi yoyote kwa ngazi za jamii.
Amesema Waswahili hao walifika Burundi zamani, lakini cha ajabu hawapewi nafasi yoyote ya uongozi wala kusikilizwa, lakini ni raia wa Burundi na wanapata taabu kutokana na kutotambuliwa kisheria.
Pia amesema Rais Mkapa aliongoza kikao kilichofanyika mwaka jana Burundi kwa kupeleka maazimio yao kwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lakini kuna mambo aliyasema ambayo hawajapendezewa nayo ingawa hakuwa tayari kuyataja, ila alisisitiza ni muhimu wao kama makundi ya vyama vyake vya siasa kusikilizwa wenyewe kwa wenyewe.
Waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia kwenye mkutano huo wa siku moja, hali iliyosababisha kutojua maazimio ya kikao hicho.

Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video



0 comments:

Post a Comment