JIJI la Mbeya limekumbwa na taharuki kwa siku mbili kutokana na tukio lililojiri katika Mtaa wa Igoma A kata ya Isanga, la mwili wa mtoto aliyekufa akiwa usingizini, kukutwa nyumbani baada ya wakazi wa mtaa huo kutoka makaburini walikokwenda kuuzika.
Mwili uliozua gumzo jijini hapa na kusababisha wakazi katika kila kona kuuzungumzia, ni wa mtoto Haruna Kyando (9).
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea juzi ambako majira ya asubuhi wazazi wa mtoto huyo, waliamka na kukuta mtoto wao amefariki na kisha kuwajulisha ndugu, jamaa na marafiki juu ya msiba uliowakuta; ambao kama ilivyo kawaida kwa misiba yote watu mbalimbali walikusanyika wakiwemo majirani.
Baada ya taratibu zote za kimsiba kufanyika, ulianza utaratibu wa kwenda kuuzika mwili huo katika makaburi ya zamani ya Isanga, ambayo kimsingi uongozi wa eneo hilo ulikwishapiga marufuku shughuli za maziko kwenye eneo hilo kutokana na kujaa na pia lina maji mengi.
Kilichowastaajabisha wakazi walioshiriki maziko hayo ni kuwa baada ya kutoka makaburini na kurejea nyumbani, waliukuta mwili wa marehemu ukiwa umelazwa kwenye godoro, kama ilivyokuwa awali kabla ya kuuingiza kwenye jeneza kwa ajili ya kwenda kuuzika.
Hapo ndipo ilipolazimu wananchi kurudi tena makaburini na kufukua kaburi na kukuta jeneza tupu likiwa halina mwili, hali iliyozusha maswali mengi, moja kati yake ikiwa ni nani aliyehakikisha kuwa mwili wa marehemu uliingizwa kwenye jeneza kabla ya kubebwa kwenda makaburini kuzika.
Kwa upande wake, wazazi wote wawili wa marehemu walisema wao hawakuelewa chochote kinachoendelea kutokana na majonzi ya mtoto wao, aliyefariki ghafla kwa ugonjwa wa kifafa.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula alisema Januari 16, mwaka huu saa nne asubuhi katika Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga Tarafa ya Sisimba, Polisi ilipokea taarifa kuwa maiti iliyokwenda kuzikwa katika makaburi ya zamani ya Isanga ilikutwa nyumbani, chumbani ikiwa kwenye godoro.
Kaimu Kamanda Lukula alisema kutokana na taarifa hiyo, Polisi walifuatilia na kubaini kuwa siku hiyo saa moja asubuhi, Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na mkewe Anna Elieza (32) wote wakazi wa Mtaa wa Igoma A, waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa kwanza, Haruna Kyando (9) amefariki dunia akiwa amelala.
Alisema taarifa za awali zilieleza kuwa Haruna tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa, hali iliyosababisha kubaki nyumbani pasipo kwenda shule kusoma.
Alisema kutokana na kifo hicho, msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika ambako majira ya saa sita mchana jeneza lililetwa msibani na kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa na blanketi na kulazwa chini kwenye godoro.
“Baada ya maombi yaliyoongozwa na waumini wa Kanisa la Kilokole Bonde la Baraka, vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha kuzikwa,” alieleza Kaimu Kamanda wa Polisi.
Alisema waombolezaji waliporudi nyumbani ndipo walitaharuki kuona mwili wa marehemu ukiwa chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.
“Kutokana na hali hiyo, taarifa zilifikishwa Polisi mara moja, askari Polisi walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu ambao kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya. “Taratibu nyingine za mazishi zitafanyika leo (jana) tarehe 17.01.2017. Mpaka sasa bado haijafahamika ni uzembe /bahati mbaya wafiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza au kulikuwa na hujuma zozote. Upelelezi unaendelea kuhusu tukio hili,” alibainisha Kaimu Kamanda.
Source:habarileo
0 comments:
Post a Comment