Wednesday, January 18, 2017

TRA yakusanya trilioni 7.27/-

MAMLAKA ya Mapato (TRA) imetangaza kukusanya kiasi cha Sh trilioni 7.27 ambayo ni makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2016 katika mwaka huu wa fedha.
Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 12.74 ukilinganisha na kiasi cha Sh trilioni 6.44 ambazo zilikusanywa katika kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita.
“Tumejiwekea malengo yetu kwa mwaka mzima ni kukusanya shilingi trilioni 15.1 kwa mwaka huu wa fedha, tayari tumeshakusanya zaidi ya nusu, tunaamini kwamba tutafika malengo tuliyojiwekea,” alisema Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
Akifafanua kuhusu makusanyo hayo, Kayombo alisema Julai walikusanya Sh trilioni 1.07, Agosti Sh trilioni 1.15, Septemba Sh trilioni 1.4, Oktoba Sh trilioni 1.13, Novemba Sh trilioni 1.12.
“Mwezi Desemba pia hatukufanya vibaya kwani tumekusanya kiasi cha Sh trilioni 1.41,” alisema Kayombo na kuongeza TRA imefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kutokana na kuweka mifumo mizuri ya ukusanyaji kodi na hivyo kupunguza kuonana kati ya mlipa kodi na ofisa wa TRA.
Alisema makusanyo pia yameongezeka kutokana na uadilifu uliopo sasa hivi kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo pamoja na kampeni ya kuwataka wananchi walipe kodi.
Kayombo alisisitiza kuwa jitihada zinafanywa ili kuhakikisha TRA inaongeza makusanyo kwa kuongeza ufanisi katika uksuanyaji, kuhimiza maadili mema kwa watumishi, kuboresha mifumo ya ukusanyaji, kushirikiana na vyombo vingine vya dola na wananchi katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kufuatilia na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki na kuhimiza ulipaji wa kodi ya majengo.
“TRA inaendelea kuhimiza wafanyabiashara wote waliosajiliwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwasilisha ritani za VAT kabla ya tarehe 20 ya kila mwezi kama ilivyobadilishwa katika Sheria ya Fedha ya 2016,” alisema Kayombo.
Alitoa mwito kwa wafanyabiashara kulipa kodi stahiki kwa hiari na wakati ili serikali ipate mapato yake.

Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video


0 comments:

Post a Comment