MAITI ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini hapo.
Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.
Haruna aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake, alikutwa na wazazi wake Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na mkewe, Anna Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii nyumbani kwao Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini hapa.
Kilichowapa taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo walikokwenda kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.
Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.
Hatua hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku hiyo hiyo ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya machozi, kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga wakishinikiza kaburi lifukuliwe.
Lakini juzi baada ya kukamilishwa kwa taratibu husika, ikiwemo kupatikana kwa kibali kutoka mahakamani, saa nne na nusu asubuhi, Polisi Mkoa wa Mbeya walifika eneo la makaburi alipozikwa marehemu na kusimamia shughuli nzima ya kufukua kaburi hilo.
Shughuli hiyo iliyodumu kwa muda wa nusu saa kama ilivyokuwa siku ya kwanza, ilihudhuriwa na mamia ya wakazi jijini hapa waliotaka kujua nini kilichozikwa ilhali mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa wakati huo.
Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.
Kutokana na hali hiyo, Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vijana, walibeba jeneza hilo na kuelekea nalo katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili kuendelea na taratibu za maziko kwa mara nyingine.
Baada ya ndugu kukabidhiwa mwili, jeshi hilo pia lilisimamia maziko yaliyofanyika upya saa 10 jioni katika kaburi lile lile la awali, lakini tofauti na awali, kabla ya kuzika ulifanyika utaratibu wa ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria, kuuaga mwili wa marehemu uliokuwa ndani ya jeneza lililofunuliwa upande wa kichwani.
Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, baadhi ya ndugu na majirani wa Mtaa wa Igoma, walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili kwa maana ya hujuma iliyofanywa kwa makusudi, ikilenga maslahi binafsi ya mtu inayohusishwa na imani za kishirikina au bahati mbaya ya kuusahau mwili wa marehemu.
Source:habarileo
0 comments:
Post a Comment