Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mchezaji wa Kagera Sugar, David Abdalla Burhan kilichotokea Hospitali ya Bugando usiku wa Januari 30, 2017.
Kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF ametuma salamu za rambirambi kwa uongozi mzima wa Klabu ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, familia ya marehemu, ndugu, jamaa, majirani na marafiki wa marehemu Burhan.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Malinzi amesema kwamba anatambua ya kuwa wakati huo ni mgumu kwa wanafamilia ya Wana Kagera Sugar na familia ya marehemu hivyo kwa wakati huu amewataka kuwa na moyo wa subira.
Taarifa za awali, zinasema kwamba kabla ya umauti, Burhan aliugua ghafla wiki iliyopita akiwa safarini kutoka Singida na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo usiku wa Alhamis.
Siku ya Ijumaa alihamishiwa Hospitali ya Kagera Sugar, na kisha kusafirishwa hadi Bugando siku ya Jumapili kwa uchunguzi zaidi. Usiku wa Jumapili, alifanyiwa vipimo na kuonekana kwamba mapafu yamejaa maji. Katika jitihada za kupatiwa matibabu alifariki saa nane za usiku wa Jumapili.
Mwili wa marehemu kwa sasa uko Bugando, na uongozi wa Timu unafanya taratibu za kusafirisha hadi nyumbani kwao Iringa.
Wakati kifo hicho kinatokea, Kagera Sugar ilikuwa kwenye maandalizi ya asilimia 100 ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara kama ilivyo kwa mgeni wake Mtibwa Sugar ambako kwa mujibu wa ratiba, ulikuwa uchezwe Januari 30, 2017.
Mchezo huo umeendelea kwa sababu viongozi wa timu zote mbili, walikubaliana kucheza ili kumuenzi marehemu Burhan; pili maandalizi yaliyokamilika na zaidi, Mtibwa Sugar tayari ilikuwa Kagera kwa ajili ya mechi hiyo.
Pia mchezo huo umeendelea baada ya familia kutangaza kuwa mazishi ni Jumatano Februari mosi, 2017 hivyo wadau kadhaa siku ya Jumanne watapata nafasi ya kusafiri kwenda Iringa, ambako wamepanga kuzika. Kanuni za Ligi Kuu, zinaahirisha mchezo kama mchezo unafanyika siku ya mazishi, lakini marehemu Burhan atazikwa Jumatano, hivyo wengi watapata fursa ya kwenda kushiriki.
Kwa sababu hizo, TFF ilibariki mchezo huo ufanyike na zaidi tumeagiza wavae vitambaa vyeusi begani na kupata dakika moja ya maombolezo. Kadhalika michezo yote ya wikiendi hii, tunaagiza wachezaji kuvaa vitambaa vyeusi na kupata dakika moja ya maombolezo kabla ya mpira kuanza.
Marehemu Burhan ni Mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pan Africa, Abdallah Burhan. Alianzia timu ya vijana wa chini ya miaka 20 ya Kagera Sugar, kabla ya kujiunga na Lipuli ya Iringa, Tanzania Prisons na Mbeya City za Mbeya, Maji Maji ya Songea na baadaye kurudi Kagera Sugar.
Mungu amlaze mahala pema.
Source:bongo5
0 comments:
Post a Comment