RAIS wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ameimwagia neema Tanzania ambapo takribani mikataba tisa inayogusa maeneo ya kilimo, afya, elimu, diplomasia, uchukuzi, habari, ulinzi na viwanda imesainiwa.
Aidha, nchi hiyo ya barani Ulaya pamoja na Tanzania zimekubaliana kuongeza thamani ya biashara baina yake kutoka dola za Marekani milioni 160 mpaka milioni 190 za sasa hadi kufikia dola za Marekani milioni 250.
Pamoja na hayo, Erdogan ameihakikishia Tanzania na Afrika kwa ujumla kuwa sera ya nchi yake kwa Afrika ni usawa na si sera zinazofurahisha upande mmoja na kuukandamiza mwingine. Marais hao wawili akiwemo Rais John Magufuli, walishuhudia mikataba hiyo tisa ikisainiwa na mawaziri wa pande zote mbili Tanzania na Uturuki Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na mkataba wa ushirikiano baina ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege Uturuki (Turkish Airline), ushirikiano baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji Uturuki na mkataba wa ushirikiano katika maendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Mikataba mingine ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu na utafiti, ushirikiano baina ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwanda vya Kati Uturuki na ushirikiano katika sekta ya utalii kwa nchi zote mbili.
Pia mikataba mingine iliyosainiwa ni ushirikiano katika viwanda na ulinzi, kwenye sekta ya afya na ushirikiano baina ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na cha Uturuki.
Mawaziri wa Tanzania walishiriki kusaini mikataba hiyo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Rioba.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Dk Magufuli alimshukuru Rais Erdogan kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea katika ziara yake Afrika, jambo lililosababisha nchi hiyo kumwagiwa neema ya mikataba tisa yenye lengo la kuboresha na kuimarisha sekta husika kwa nchi zote mbili.
“Katika kabila langu kuna methali inayosema ukiwa wa kwanza kunywa maziwa maana yake utakunywa mengi zaidi. Hili limejidhihirisha kupitia mikataba hii tuliyotiliana saini itakayonufaisha zaidi Tanzania,” alisisitiza Dk Magufuli.
Alisema hivi karibuni Tanzania imeteua Balozi wa Tanzania nchini Uturuki kwa mara ya kwanza, Profesa Elizabeth Kiondo, ikiwa ni ishara na msingi imara kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hasa katika kushirikiana kibiashara na kiuwekezaji.
Rais Magufuli alisema anaamini kupitia ushirikiano huo mpya wa kidiplomasia nchi hizo zitaimarisha zaidi uhusiano wake kwa upande wa maendeleo kwani tayari katika mazungumzo aliyoyafanya na Rais Erdogan amemuomba kupitia Benki ya Exim ya Uturuki kuikopesha Tanzania fedha zitakazotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa.
“Tanzania tuko kwenye mchakato wa ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganisha nchi yetu na nchi nyingi za jirani. Kwa sasa tupo kwenye hatua ya kutafuta mkandarasi na nafahamu moja ya kampuni kutoka Uturuki imeomba kuijenga reli hii. Tuombe Mungu mfanikiwe katika hili,” alisema Dk Magufuli.
Source:habarileo
0 comments:
Post a Comment