MWENYEKITI mpya wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage amesema atafanya kazi yake kwa uadilifu mkubwa na kwa kufuata sheria, kanuni na Katiba ya nchi.
Akizungumza Dar es Salaam jana na gazeti hili, Jaji Kaijage ambaye uteuzi wake ulitangazwa jana na Ikulu, alisema taasisi anayoenda kuifanyia kazi inaendeshwa kwa sheria za uchaguzi na katiba ya nchi.
“Kwa kweli niahidi utendaji unaozingatia sheria na katiba ya nchi, nitafuata sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza Tume ya Uchaguzi,” alisema Jaji Kaijage, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Ataiongoza NEC kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Desemba 20, mwaka huu.
Jaji Kaijage alitoa msimamo huo baada ya gazeti hili kumuuliza namna gani ataitumikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo imekuwa inalalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa kuwa haiko huru kutokana na watendaji wake kuteuliwa na Rais, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala.
“Hakuna namna nyingine ya kumpata mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kwa sasa hivi, lazima katiba iongoze anapatikanaje, sio kwa sababu nataeuliwa na Rais kwamba nitapindisha taratibu, hapana, nitafuata sheria na katiba,” alisisitiza Jaji Kaijange, ambaye hata hivyo hakutaka kuingia kwa undani, kwa maelezo kuwa hajaapishwa kushika wadhifa huo.
Uteuzi wa Jaji Kaijage ambao umefanywa na Rais John Magufuli, ulitangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi. Jaji Kaijage amekuwa Mwenyekiti wa NEC akichukua nafasi ya Jaji mstaafu Damian Lubuva, ambaye muda wake wa kuwa mwenyekiti wa Tume hiyo, umemalizika hivi karibuni.
“Jaji Semistocles Kaijage anachukua nafasi ya Jaji mstaafu Damian Lubuva ambaye muda wake wa kuwa Mwenyekiti umemalizika rasmi mnamo tarehe 19 Desemba 2016,” alieleza Balozi Kijazi katika taarifa yake hiyo, iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Dar es Salaam. Wasifu wake Jaji Kaijage alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, wadhifa alioushikilia kuanzia mwaka 2012.
Alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu kuanzia mwaka 2000 ambapo amewahi kuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dodoma (2004-2006, Iringa (2006-2007) na Dar es Salaam (2007-2012).
Kabla ya hapo, alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu mwaka 1988-89. Wakati huo pia alikuwa mkuu wa mafunzo wa idara ya mahakama. Amewahi kuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa mwaka 1990-1992.
Kabla ya hapo, Jaji Kaijage amewahi kuwa Hakimu wa mahakama mbalimbali nchini; na alipanda kuwa Jaji wakati huo akiwa Hakimu Mkuu Mkazi.
Alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Bihawana mkoani Dodoma mwaka 1970-1973; na baadaye alijiunga na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Mkwawa, Iringa mwaka 1974 hadi 1975.
Mwaka 1979 -1982 alisoma Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada yake ya Uzamili alisomea Chuo cha Cardiff cha Chuo Kikuu cha Wales, Uingereza.
Uteuzi mwingine
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua tena Jaji mstaafu Hamid Mahamoud Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC kwa kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia juzi, Desemba 20, mwaka huu.
Jaji Hamid alikuwa katika nafasi hiyo, kabla ya uteuzi huo kwa miaka mitano. Muda wake kuwa katika nafasi hiyo ulikwisha Desemba 19, mwaka huu.
Halikadhalika, Rais Magufuli pia amemteua Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Harold Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Desemba 20, mwaka huu.
“Jaji mstaafu Nsekela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji mstaafu Salome Kaganda ambaye amestaafu mnamo tarehe 10 Desemba, 2016,” ilieleza taarifa hiyo jana.
Majaji 4 wapya
Mahakama ya Rufaa Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewateua majaji wanne wa Mahakama Kuu kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia jana.
Majaji hao ni Dk Gerald Ndika, Jackobs Mwambegele, Rehema Kiwanga Mkuye na Sivangilwa Mwangesi. Wateule wote hao, waliotajwa katika taarifa hiyo ya Ikulu, wataapishwa leo tarehe 23 Desemba, 2016 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Source:habarileo
Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video
0 comments:
Post a Comment