Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora za nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), leo zimekutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kutathmini utekelezwaji wa mpango kazi wa haki za binadamu unaomaliza muda wake mwaka huu.
Mpango kazi huo wa miaka mitatu ulianza kutekelezwa mwaka 2014.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mary Massay amesema pia mkutano huo utatumika kujadili namna ya kuondoa vyanzo vya migogoro hasa ya kisiasa, kikabila na ya ardhi katika nchi wanachama wa EAC.
“Mkutano huu ni wa siku tatu, wenye lengo la kufanya tathimini ya mpango kazi wetu wa miaka mitatu ulioanza kutekelezwa mwaka 2014 na kwamba unaisha mwaka huu. Pia Tume zetu zitajikita kufanya utafiti wa namna ya kuondoa vyanzo vya migogoro kwa sababu haki za binadamu haziwezi patikana ikiwa hakuna amani,” amesema.
Ameongeza kuwa “Tunataka kuona kwamba katika miaka mitatu kumekuwa na hali gani ya haki za binadamu, kuona tumefanya vizuri au kuna mahala tuongeze jitihada maana haki za binadamu ni pana, kuna haki ya kuishi, kuwa salama. Pia tutajadili namna ya kuongeza jitihada za utolewaji elimu kwa wananchi ili kila mtu azingatie haki za binadamu.”
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome baada ya kuufungua mkutano huo, amewataka washiriki wake kutekeleza maazimio yatakayoafikiwa.
“Wataalamu watajadili mambo ya haki za binadamu, migogoro katika eneo la afrika mashariki, pia watabadlishana mawazo kupata njia muafaka za kusuluhisha migogoro na kudumisha utekelezwaji wa haki za binadamu.” amesema na kuongeza.
“Maazimio watakayofanywa yawe maazimio yanayolenga kutatua changamoto za haki za binadamu tulizonazo.”
Source:dewjiblog
0 comments:
Post a Comment