Wednesday, November 2, 2016

Rais Magufuli ampongeza Rais Kenyatta kwa ujenzi wa barabara ya kisasa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta wamezindua barabara ya Southern Bypass huku Rais Magufuli akisema wananchi wanahitaji maendeleo na hayo ndio yenyewe.


Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Magufuli amempongeza Rais Kenyatta na serikali yake kwa kujenga barabara hiyo ambapo amesema haitawasaidia wananchi wa Kenya tu, bali pia itawasaidia wananchi wa Afrika Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.

“Wananchi wanahitaji maendeleo na haya ndio maendeleo, barabara hii itasaidia kuinua uchumi na itasaidia masuala ya kijamii,” alisema Rais Magufuli.
Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 28 na inaunganisha maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi. Uzinduzu huo umefanyika katika eneo la Karen nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Dkt. Magufuli amesema viongozi wa Afrika Mashariki wameamua kufanya kazi ya kuharakisha maendeleo na kuinua maisha ya wananchi, na kwamba ili kufanikisha hilo wamedhamiria kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara zinazounganisha nchi wanachama na kujenga vituo vya pamoja vya utoaji wa huduma za mpakani (One Stop Border Post).
Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi na pia kutaboresha shughuli za maendeleo ya wananchi.
Mhe. Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana nae kuzindua barabara hiyo na amesema Kenya itaongeza juhudi katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa barabara zinazounganisha Kenya na Tanzania zikiwemo barabara ya Malindi kupitia Saadani hadi Bagamoyo nchini Tanzania na barabara ya Voi – Taveta- Holili-Arusha.Sherehe za uzinduzi wa barabara ya Southern By-pass zimehudhuriwa na Naibu Rais wa Kenya Mhe. William Ruto.

Kabla ya kuzindua barabara hiyo Rais Magufuli ametembelea kiwanda kidogo cha kusindika maziwa cha Eldoville kilichopo katika eneo la Karen ambacho kinamilikiwa na familia ya mkulima Bw. James Karuga.
Familia hiyo ilianzisha kiwanda cha kusindika maziwa mwaka 1985 kwa uzalishaji wa chini ya lita 1,000 kwa siku na hivi sasa imefikia uzalishaji wa lita 5,000 kwa siku na inatarajia kuongeza uzalishaji hadi lita 70,000 katika mwaka mmoja ujao baada ya kuongeza kiwanda cha pili.




Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video




0 comments:

Post a Comment