Monday, November 7, 2016

MIAKA 74 MILIMA, MABONDE YA SAMUEL SITTA

Buriani Samuel Sitta kiongozi mwenye historia kubwa kwa taifa la Tanzania; uhodari wako kwa WanaUrambo kamwe hautafutika vichwani mwa wananchi hao. Ingawa haikuwa kazi rahisi kuwatumikia kwa miaka yote hiyo lakini wataendelea kukukumbuka na kuyaenzi yale mema uliyowaachia kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa.

Ninachokikumbuka kuhusiana na Sitta ni namna alivyoweza kuliendesha kwa umahiri mkubwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 2005 hadi 2010 na kumkabidhi kijiti Spika Mstaafu Anne Makinda aliyeshikilia usukani kuanzia 2010 hadi 2015 nae akakabidhi mikoba kwa Spika wa sasa Job Ndugai.

Pia utakumbuka namna Hayati Samuel Sitta alivyofanya kazi kubwa mwaka 2014 alipokuwa Mwenyekiti wa Kudumu Bunge la Katiba ili kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba na kuwa na Katiba Inayopendekezwa licha ya changamoto alizokumbana nazo.

Hakuishia hapo pia alijitokeza katika mbio za urais kutangaza nia na kuomba ridhaa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa nafasi ya urais mwaka 2015 ingawa hakufanikiwa kupita.

Lakini jambo ambalo bado linaishi vichwani mwa Watanzania ni pale Samuel Sitta alipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974 kwa masomo ya Shahada ya Sheria (LLB) alikumbana na kadhia ya viboko vya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama sharti la kurejea chuoni hapo baada ya kutimuliwa kwa kile kilichodaiwa Sitta na mwenzie Wilfred Mwabulambo ambaye pia ni marehemu kuwa vinara wa mgomo chuoni hapo.

Kila binadamu ana magumu na changamoto zake na hata njia ya mafanikio baina ya mtu na mtu pia hutofautiana; Samuel Sitta amelala kwa sasa, tena amelala usingizi wa milele baada ya kusumbuliwa na maradhi ya saratani ya tezi dume iliyosambaa miguu na kuathiri mwili mzima. Wakati umefika kwa Watanzania kwa ujumla kuungana na familia katika kipindi hiki kigumu kuwafariji na kuyaenzi yale mazuri aliyoyaacha.




Source:mtembezi

Jiunge na hatukwamii.blogspot.com/ sasa


Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video







0 comments:

Post a Comment