Monday, October 3, 2016

Mtoboa macho wa Buguruni Sheli atiwa mbaroni

Kamanda wa polisi kanda maalum ya mkoa wa Dar es Salaam, Simon Sirro amesema jeshi lake limemkamata mtuhumiwa ‘Scorpion’ anayetuhumiwa kuhusika katika tukio la kumtoa  macho, kumchoma visu na kumpora mfanyabiashara Said Ally katika maeneo ya Buguruni Sheli.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akimsikiliza Said Ally akisimulia jinsi alivyotobolewa macho

Kamanda Sirro ametoa kauli hiyo Jumapili hii Buguruni kwa Mnyamani, jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa kujadili usalama katika eneo hilo ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Alisema mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina maarufu kama ‘Scorpion’ alikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa za matukio ambayo ameyafanya ikiwemo la kumchoma kisu, kumtoa macho na kumsababishia upofu, Said Ally.
“Nimesikia wananchi wanalalamika hapa kuwa tumeshindwa kumkamata Scorpion, ni nani kwa Jeshi la Polisi asikamatwe? Tayari tumemkamata na sheria itachukua mkondo wake, hakuna mtu anayeweza kushindana na jeshi,” alisema Kamanda Sirro.
Aidha Sirro alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo na kuhojiwa aliutaja mtandao wake wote na tayari wameukamata. Awataka wakazi wa eneo hilo kutokuwa na hofu kwani mtuhumiwa huyo hayupo tena katika eneo hilo.
“Najua suala hili bado lipo mahakamani hatuwezi kulizungumzia sana, bahati nzuri alipokamatwa alieleza aliyoeleza na tukafanikiwa kuukamata mtandao wote, hivyo hakuna haja ya kuwa na uwoga eneo hili lipo salama,” aliongeza.
BY: EMMY MWAIPOPO

0 comments:

Post a Comment