Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imekaribisha uwekezaji zaidi kwenye sekta ya Bima nchini ili kuibua ushindani utakaochochea ubunifu wenye tija zaidi kwa wadau wa sekta hiyo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kampuni mpya ya Bima ijulikanayo kama Clarkson Insurance Brokers Tanzania Limited, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF , Bw. Godfrey Simbeye alisema ustawi wa uchumi wa nchi kwa sasa unahitaji uimara na ubunifu zaidi kwenye sekta ya bima hivyo wingi wa kampuni hizo unaweza kuwa na tija zaidi katika kufanikisha hilo.
“Tanzania kwa sasa ipo kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa kama ile ya bomba la mafuta, ujenzi wa reli ya kati, ujenzi wa barabara na majengo makubwa ya kisasa, vyote hivi vinahitaji kulindwa na bima hivyo ujio wa kampuni kama hii ya Clarkson Insurance Brokers Tanzania Limited tunauona kama ni heri na wenye tija kwa taifa,’’ alibainisha.
Kwa mujibu wa Bw Simbeye kwa sasa mchango wa sekta ya Bima kwenye Ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ni chini ya asilimia 1 huku akiitaja sekta binafsi kuwa ni miongoni mwa sekta ambazo bado hazijafaidi ipasavyo matunda ya uwepo wa huduma za Bima ambapo alitaja suala la ukosefu wa ubunifu miongoni mwa makampuni ya Bima kuwa ni moja ya sababu ya uwepo wa changamoto hiyo.
“Matumaini yangu kwa kampuni ya Clarkson Insurance Brokers Tanzania Limited kwa kiasi kikubwa yanachochewa na ukongwe wao wa miaka 58 wakitoa huduma hii nchini Kenya ikiwa ni pamija na Uganda hivyo natarajia kwamba uzoefu wao katika kipindi hicho kirefu unaweza kuwa na tija zaidi hapa nchini,’’ aliongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa makampuni ya Bima ya Clarkson Insurance Brokers Tanzania Group Bw Justin Lambert alisema pamoja na kutoa huduma kwa weledi, kampuni yake itajikita zaidi katika kutoa elimu ya bima kwa jamii ili kuwavutia zaidi wengi ambao kwasasa bado hawajaingia kwenye huduma hiyo.
“Clarkson Insurance Brokers hatujaingia hapa nchini ili kuongeza idadi ya makampuni ya bima yaliyopo nchini bali lengo letu hasa kuongeza ushindani na kuleta mapinduzi makubwa na yenye tija kwa wadau wa sekta hii muhimu,’’ alibainisha.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo hapa nchini Bw, Patrick Marimo alisema mafanikio ya kampuni hiyo katika soko lake jipya hapa nchini kwa kiasi kikubwa yatachochewa na ubunifu mkubwa wa kampuni hiyo katika utoaji wa huduma zake.
“Tunalenga kuleta mabadiliko makubwa kwenye huduma hii muhimu na ndio maana pamoja na mambo mengine tutajikita zaidi katika kutoa elimu kwa jamii ili kuijengea uelewa zaidi kwenye masuala ya bima ili tutoe huduma kwa watu wenye uelewa zaidi …lakini pia uwekazaji wetu kwenye teknolojia ya kisasa unaweza kuwa chachu zaidi katika kufikia malengo,’’ alisema.
Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Kampuni ya Clarkson Insurance Brokers inayojishughulisha na masuala ya bima Bw.Godfrey Simbeye ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF akionyesha zawadi aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Clarkson Insurance Brokers Justin Lambert mara baada ya uzinduzi wa kampuni hiyo uliofanyika kwenye hoteli ya Hyyat Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Parkal Randall ambayo ni Kampuni Tanzu ya Clarkson Insurance Brokers Bw. Coutts Otolo akiwatambulisha watendaji wa mbalimbali wa kampuni hiyo.
Mwanamuziki John Muhina kulia akiimba pamoja na wanamuziki wenzake wa bendi ya Tanzanite Band katika uzinduzi huo.
0 comments:
Post a Comment