Skip to content
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ametoa mwito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi nchini kuimarisha ulinzi katika eneo la pwani ya Mashariki ya kisiwa cha Unguja ambako shughuli nyingi za kitalii zinafanyika.
Alitoa mwito huo jana wakati alipozungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliyemtembelea ofisini kwake Ikulu mjini Zanzibar.
“Umelieleza vyema suala la ulinzi wa pwani ya nchi yetu, lakini huku Zanzibar tuna biashara ya utalii na ukanda wa pwani ya Mashariki ambako kuna huduma nyingi za biashara hiyo uko wazi sana na ulinzi wake ni hafifu,” Dk Shein alimueleza waziri huyo.
Awali, Mwigulu alimueleza Rais Shein kuwa katika kipindi hiki na kijacho wizara yake inaelekeza suala la ulinzi wa pwani ya nchi kuwa la muhimu hasa ikizingatiwa suala la uendelezaji wa sekta ya gesi na mafuta katika ukanda wa pwani ya nchi yetu.
Katika hatua nyingine, Dk Shein alimueleza waziri huyo wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na ajali za barabani pamoja na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya askari wa usalama barabarani ambavyo ni kinyume na maadili ya kazi zao.
0 comments:
Post a Comment