RAIS John Magufuli amewaagiza viongozi wa mkoa wa Morogoro na Manispaa, kuwaacha wafanyabiashara ndogo waendelee kufanya biashara kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Msamvu.
Rais Magufuli aliyatoa maagizo hayo jana baada ya msafara wake kutokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam, kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu. Wananchi hao walimweleza Rais Magufuli kuwa wananyanyaswa na viongozi wa Manispaa hiyo, kwa kuwafukuza wasifanye biashara tangu kituo cha mabasi Msamvu kijengwe upya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli pia alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei kuhakikisha kwamba askari mgambo hawawasumbui tena wafanyabiashara hao.
Pamoja na kumuagiza Kamanda Matei kuchukua hatua hiyo, Rais pia aliwataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri wa kufanya biashara eneo hilo unaandaliwa kwa ajili yao.
Aidha, Rais Magufuli amewataka watu wote walioshindwa kuviendeleza viwanda vilivyobinafsishwa kwao, kuvirejesha serikalini ili wapewe wawekezaji wenye uwezo wa kuviendeleza na kuzalisha ajira.
“Ninarudia mwito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwawameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), narudia akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” alisisitiza Rais Magufuli.
Kuhusu kilimo, Rais Magufuli aliwapongeza wakulima wa mazao mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na hasa wakulima wa wilayani Kilosa, ambao wameongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 kwa msimu wa kilimo uliopita hadi kufikia asilimia 82 msimu huu.
Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Morogoro, kuchangamkia ajira kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge), lakini amewataka watu waliojenga kweye hifadhi ya reli kuanza kubomoa majengo hao kwa hiari.
Baada ya kuondoka Morogoro aliwasili jijini Dar es Salaam majira ya mchana, ambapo akiwa katika eneo la Tegeta Wilaya ya Kinondoni, alizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Tegeta, nianze kwa kuwashukuru sana, kwa kura nyingi mlizonipa ili niwe Rais wa Awamu ya Tano, nawashukuru CCM, nawashukuru CHADEMA, nawashukuru CUF, nawashukuru ACT na hata wale ambao hawana chama kwani wote kwa umoja wenu mlitanguliza maslahi ya Taifa na kumpa kura mtu ambaye atalisaidia Taifa, na mimi nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili Watanzania wote hasa wanyonge ambao siku zote walikuwa wakionewa,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitaja baadhi ya mambo tangu aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Sh bilioni 371 hadi kufikia Sh bilioni 483, kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.
“Kwenye madini tumeibiwa sana, nchi yetu ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuibiwa, tumeibiwa kwa miaka 18, sasa imetosha,” alisema. Aidha Rais Magufuli ameipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuzuia udahili wa wanafunzi wote wa mwaka kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia udahili wa wanafunzi wa kozi 75 katika vyuo vikuu 22 kutokana na dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo hivyo uliofanyika Oktoba 2016
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment