Thursday, June 15, 2017

Mo Dewji Azidi Kufanya Kufuru Simba Sc..Awaambai Viongozi Wasajili Pesa Kwake Siyo Tatizo.

SASA hii ni jeuri ya fedha, kwani baada ya Simba kufanikiwa kuzinasa saini za John Bocco, Shomari Kapombe na kipa Aishi Manula kutoka Azam FC, mwanachama maarufu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameuambia uongozi utafute wachezaji wengine wazuri, kwani fedha kwake si tatizo.


Mbali na wachezaji hao watatu kutoa Azam FC, pia Simba imefanikiwa kuzinasa saini za mabeki wawili, Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC pamoja na Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans, zote za jijini Mwanza, na Mo amesema anataka waletwe wengine wenye uwezo mkubwa zaidi.

Gazeti la Dimba limenasa ujumbe wa Mo ukiwataka Wanasimba kuwa kitu kimoja, huku akisisitiza kwamba lazima ufanyike usajili wa nguvu ili timu irudishe heshima yake iliyopotea kwa misimu kadhaa.

“Narudisha heshima ya Simba SC iliyopotea ndani ya misimu mitatu, pesa si tatizo kwangu, usajili huu ni chachu ya Simba kuelekea kwenye mafanikio endelevu na kufanya vyema kimataifa, huu ni muda mzuri kwetu kuunganisha nguvu zetu zote kuona Simba SC inafanikiwa na kuliletea heshima taifa letu, Simba nguvu moja,” ulisomeka ujumbe huo.

Kauli hiyo ya Mo inaupa uongozi jeuri ya kuinasa saini ya mastraika hatari kutoka nje ya nchi, akiwamo yule straika wa Zambia, Walter Bwalya, ambaye ana njaa ya mabao kinoma.

Aidha, Mo, ambaye ameonekana kujiamini sana, amewahakikishia Wanasimba kwamba mbali na huyo, pia straika mwenye zali na Simba, Emmanuel Okwi, wanamalizana naye kila kitu ndani ya siku mbili hizi na atatua Msimbazi dakika yoyote kuanzia sasa, huku pia klabu hiyo ikikamilisha mazungumzo na straika wa AFC Leopards, Allan Kateregga, ambaye wamekuwa wakimfukuzia baada ya kuona uwezo wake katika michuano ya SportPesa, iliyomalizika hivi karibuni Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.





Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment