KAMPUNI ya Barrick Gold Corporation, ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited, imesema ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha, ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited, Prof John Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
Prof Thornton ambaye alisafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania, alikutana na Rais Magufuli, jana Ikulu, na mazungumzo yao yalihudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini, Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi. Baada ya mazungumzo hayo, Profesa Thornton alisema kuwa kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania, yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote, ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo; na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa; na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
Rais Magufuli alisema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa, Profesa Thornton alikubali kushirikiana na Tanzania, kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment