UTEUZI wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi, umewafanya baadhi ya watu akiwamo mtangulizi wake Kamishina mstaafu wa Polisi, Suleiman Kova kutoa waliyo nayo.
Katika mazungumzo na gazeti hili kwa nyakati tofauti, watu wa kada mbalimbali walielezea namna wanavyomjua Sirro huku wengine wakimpa kazi na kumtajia wayajuayo. Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Severine Niwe- Mugizi (pichani) alimwomba IGP Sirro kutumia weledi wake kuutazama kwa makini Mkoa wa Kagera hususani Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara linalobeba wilaya za Ngara, Biharamulo na Chato kwa kuanzisha mkoa au kanda maalumu ya kipolisi kwa kuwa ni eneo hatarishi kwani linapitika kirahisi na watu kutoka nchi jirani wakiwamo wakimbizi.
“Haya ni maeneo hatarishi, magumu na yenye changamoto nyingi maana ni mpakani mwa nchi ambazo mara nyingi zina matatizo ya amani na usalama japo tunasema kuna amani na utulivu katika nchi hizo,” alisema.
Akaongeza, “Mwingiliano rahisi uliopo unatuweka kwenye hatari tusiyopaswa kuendelea kuipuuza wala kusubiri jambo lifumuke eti ndipo tuanze kuwa makini na kufuatilia vilio vilivyopuuzwa siku nyingi.
Mimi nimkaribishe Sirro kwa kumuomba kwa dhati kabisa eneo hili aliundie kanda maalumu ya kipolisi.” Alisema, “Ninaamini silaha nyingi haramu zinazoingia na kufanya uhalifu nchini, zinapitia maeneo hayo.”
Kwa upande wake, Kamishina mstaafu wa Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyempisha Sirro nafasi ya Ukamanda wa Kanda alisema ni wajibu wa wananchi na askari Polisi katika ngazi zote, kumpa ushirikiano wa kutosha IGP Sirro apambane na kuzishinda changamoto zilizo mbele yake.
“Sirro achukue kijiti cha Mangu, aangalie zile changamoto ambazo Mangu alikuwa hajazikamilisha, yeye sasa azikamilishe.” Alipoulizwa anavyomfahamu Sirro kiutendaji kwa kuwa Sirro amewahi kufanya kazi chini yake akiwa Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kova alisema, “Ninachokifahamu kwa Sirro ni kwamba, ni msikilizaji wa watu, mwelewa wa mambo, mtiifu na mtekelezaji mzuri wa maelekezo na maamuzi.
Huyu jamaa ni hodari kwa ufuatiliaji na utekelezaji.” Mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Wamachinga Tanzania (Shiuma-Tz), Matondo Maganga, alisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuutambua utendaji kazi wa Sirro huku akisisitiza kuwa, ni mtu makini, anayezingatia haki na asiyependa uonevu, wala mambo ya gizani.
“Kwa kweli Sirro ni askari wa ajabu; anatetea na kuzingatia haki na utu wa mtu, hana konakona, na ni mtu mwenye saikolojia kali… Anaweza kumwita mhalifu, wakazungumza na kisha akamwambia nenda, hiyo ni adhabu kubwa ambayo ni chanya na imewasaidia na kuwabadili wengi kitabia bila madhara,” alisema Matondo.
Matondo alisema wanamtambua IGP Sirro kama Mwasisi na mlezi wa Shiuma-Tz tangu alipozindua shirika hilo Aprili 22, 2010 jijini Mwanza. Mkazi wa Pugu Kajiungeni Dar es Salaam, John Igotti alisema anamfahamu Sirro kama askari shupavu anayesimamia haki, na ukweli na ni askari mtulivu na makini.
“Nasikia alikaribia kabisa kuvaa joho la upadri… Ni aina ya askari ambaye ni mlokole kwa matendo yake ndiyo maana hapendi uonevu wala kupindapinda mambo,” alisema Igotti na kumshauri kuongeza mafunzo ya kisasa kwa askari Polisi ili waendane na changamoto za uhalifu zilizopo sasa zikiambatana na matumizi ya sayansi na teknolojia.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment