MUUNGANO wa Vyama vinavyopambana kupunguza ajali barabarani umesema ajali iliyoua watoto 33 katika shule ya Lucky Vincent, ya jijini Arusha ni pigo kubwa na masikitiko na kutoa pole kwa wazazi na wenyeji wa jiji hilo la Arusha.
Umesema ajali ni changamoto kubwa kwa sekta ya usafirishaji nchini na kutokea kwa ajali hiyo, ichukuliwe kwa uzito kwa wadau mbalimbali kuongeza nguvu za kudhibiti ili barabarani pawe salama. Katibu wa muungano huo, Hassan Mchanjama, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia kuhusu kugawa vifaa vya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule zilizoko katika maeneo hatarishi ili kuweza kuvuka barabara kwa usalama.
Alisema ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani kimataifa iliyoanza jana hadi Mei 14, Muungano huo kuanzia leo utagawa vifaa pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi ili waweze kuwa salama wakati wa kuvuka barabara. Kuhusu tukio la wanafunzi wa Lucky Vincent alisema ni ajali inayotakiwa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa, na kuwaasa wamiliki wa shule kuwatumia madereva wenye kuzingatia maadili ya kazi zao kwa ajili ya usalama barabarani.
“Tunatoa pole kwa wakazi wa Arusha, ni pigo kubwa sana nchini, pole nyingi kwa wazazi, mkuu wa mkoa na hata serikali kwa ujumla,” alisema Mchanjama na kuongeza kuwa kutokana na masikitiko hayo iwe fursa ya kusimamiwa kwa dhati sekta ya usafirishaji ili majanga kama hayo yasijirudie. Kuhusu tukio la kutoa vifaa vya usalama barabarani kwa shule jijini Dar es Salaam, Mchanjama alisema katika siku ya kilele cha siku ya usalama barabarani ambapo ni Mei 12, 2017, Muungano huo utafungua klabu ya usalama barabarani katika shule ya msingi Kibamba pamoja na kutoa vifaa vya kuvukia barabara.
Alizitaja baadhi ya shule nyingine ambazo zitapewa vifaa hivyo kuwa ni pamoja na shule ya msingi ya mwalimu Nyerere, Mwembechai, Mkombozi, Bunju A, Azania, Turiani, Ubungo Kibangu, Mbezi, Jangwani, Jitihada na Yombo Dovya. Alisema Tanzania ni waathirika wa majanga ya ajali za barabarani na kuiomba serikali kushirikisha wadau wa kimataifa ili kutoa ushauri wa namna ya kukabiliana na suala hilo.
Mwenyekiti wa Muungano huo, Alpherio Nchimbi, alisema katika maadhimisho hayo, Muungano huo unaiomba serikali kuharakisha marekebisho ya sheria ya usalama barabarani ili kutoa faini kubwa ama kifungo cha muda mrefu kwa atakayehusika na kusababisha ajali.
source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.
0 comments:
Post a Comment