Friday, April 21, 2017

Magufuli kupeleka walimu wa Kiswahili Rwanda

RAIS John Magufuli ameahidi kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo, baada ya Rwanda kuamua Kiswahili kianze kufundishwa katika shule zake.
Rais alisema hayo alipopokea barua yenye ujumbe wa Rais Paul Kagame wa Jamhuri wa Rwanda, iliyowasilishwa kwake na Mjumbe Maalumu ambaye ni Waziri wa Elimu wa Rwanda, Dk Musafiri Malimba.
Pamoja na kupokea barua hiyo, Rais Magufuli na Dk Malimba walizungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda, ikiwemo katika sekta ya elimu hususani maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Magufuli aliipongeza Rwanda kwa kuamua lugha ya Kiswahili kianze kufundishwa katika shule zake na alisema Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha hiyo. Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na wafanyakazi kwa manufaa ya Taifa. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema pamoja na kuimarisha ushirikiano huo, Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wowote, utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi, wenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.
Rais Magufuli alisema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana nazo, kama ambavyo imeanza kufanya hivyo.
“Nataka kuwahakikishia nyinyi viongozi wa TUCTA na wafanyakazi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, inawapenda wafanyakazi na ipo tayari kuwapigania, jambo la msingi tutangulize maslahi ya Taifa, kawaambieni wafanyakazi wachape kazi na Serikali itawalinda” alisema Rais.
Kwa upande wao, viongozi wa TUCTA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokya walimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali yake, kujenga uchumi imara, kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa watumishi hewa na kulipa madeni ya watumishi.
Viongozi hao waliahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki na wajibu wa wafanyakazi. Waliomba Serikali iendelee kufanyia kazi masuala mbalimbali ya wafanyakazi, ikiwemo kuwalipa stahili zao na kuboresha mazingira ya kazi

source:habarileo
Tuandikie Maoni Yako Hapa Chini. Usikose kujiunga naYoutube kuangalia video za kufurahisha na kuvunja mbavu.

0 comments:

Post a Comment